Na.Mwandishi Wetu,Timesmajir
WANACHAMA wa Chama cha Mawakala wa Usafirishaji Mizigo Tanzania (TAFFA) wamepitisha utekelezaji wa Mfumo wa Tanzania Clearing Agents Minimum Agency Fee System (TCAMS), baada ya majadiliano ya kina kuhusu mkataba wa utekelezaji wa mfumo huo kati ya TAFFA na Capital Pay International.
Katika mkutano huo, wanachama walipata nafasi ya kusomewa mkataba, kuuliza maswali na kutoa maoni kuhusu mfumo huo, ikiwemo masuala ya makato ya fedha, gharama za uendeshaji na utaratibu wa utekelezaji.
Baada ya kupokea ufafanuzi, zaidi ya wanachama 300 walipiga kura kuunga mkono mfumo huo, huku wanachama watano pekee wakipiga kura za kutounga mkono, hatua inayoonesha uungwaji mkono mkubwa wa wanachama waliohudhuria mkutano huo.
Miongoni mwa masuala yaliyofafanuliwa ni kwamba fedha za wanachama hazitakatwa kupitia mfumo huo, gharama za mfumo hazitatokana na ada za huduma za uwakala (Agency Fees), na makato ya asilimia 30 yaliyokuwa yakitajwa awali si sehemu ya utaratibu uliowasilishwa kwa wanachama.

Rais wa TAFFA, Edward John Urio, amesema uongozi wa chama umejipanga kulinda maslahi ya wanachama, kuhakikisha uwazi katika utekelezaji wa mfumo huo na kuzingatia matakwa ya kisheria yaliyowekwa na Serikali kupitia Tangazo la Serikali (GN) Na. 83 la mwaka 2026.
Amesema mfumo huo unalenga kuimarisha uwazi na uwajibikaji katika sekta ya clearing and forwarding, hususan katika kuripoti na kutangaza ada za huduma, sambamba na kuhakikisha viwango vya chini vya ada vinazingatiwa kwa mujibu wa sheria.

Urio aliongeza kuwa matumizi ya mifumo ya kidijitali yatasaidia kuboresha utendaji wa sekta hiyo na kupunguza athari zinazoweza kujitokeza kutokana na kutokuzingatia matakwa ya kisheria.
Kupitishwa kwa TCAMS kunatarajiwa kuwa hatua muhimu katika juhudi za TAFFA za kuimarisha mifumo ya kielektroniki, kulinda maslahi ya wanachama na kuongeza uwazi katika utoaji wa huduma za clearing and forwarding nchini.


More Stories
Barabara za lami Mtumba kufungua njia huduma Serikalini
Kawaida atoa ufafanuzi majukumu ya Chipukizi,Vijana CCM
Viongozi makazini watakiwa kutambua michango ya watumishi wao kwa kuwapatia motisha