*Yazindua safari ya Mwanza-Dodoma,
Judith Ferdinand,Timesmajira Online-Mwanza
IMEELEZWA kuwa dira ya Serikali ni kuifungua nchi kiuchumi,kiviwanda na kibiashara huku usafiri wa anga ukiwa ni nguzo muhimu katika kufikia azma hiyo.
Katika kuunga mkono juhudi hizo Shirika la Ndege Tanzania(ATLC), limepanua wigo wa utoaji huduma kwa kuanzisha safari kati ya Mwanza -Dodoma,ambayo ilianza Juni 5,2026,itakayosaidia wafanyabiashara,wananchi na viongozi kusafiri kwa urahisi,haraka na salama kati ya miji hiyo mikuu miwili ya kimkakati.

Akizungumza Juni 19,2026 katika halfa ya uzinduzi rasmi wa safari ya ndege ya Air Tanzania kutoka Mwanza kwenda Dodoma,uliofanyika uwanja wa ndege Mwanza, Meneja wa ATCL kituo cha Mwanza Paskas Samwel amesema,hadi kufikia Juni,wameshuhudia ongezeko la safari tatu mpya kupitia mkoa huo ikiwemo ya kupitia Geita, Kilimanjaro na hiyo ya Dodoma.
Samwel amesema,ongezeko la safari hizo mpya linafanya jumla ya miruko katika ukanda huo kufikia 160 kwa mwezi,kukiwa na wastani wa ndege tano mpaka saba kwa siku.Hivyo kuongezeka kwa miruko hapa Mwanza ni uthibitisho wa ukuaji wa uchumi wa Kanda ya Ziwa.
“Tunajivunia kuona kuwa kituo hiki cha Mwanza kwa sasa kinahudumia abiria 1,000 hadi 1,300 kwa siku.Ongezeko la safari ya Mwanza-Dodoma ambayo inafanyika kwa siku mbili Ijumaa na Jumapili imeiwezesha ATCL kufikia miruko zaidi ya 32 kwa siku katika vituo vyake mbalimbali ndani na nje ya nchi,”amesema Samwel.
Pia amesema,hivi karibuni ATCL inatarajia kuanzisha safari za Musoma na Shinyanga,Moscow nchini Urusi Julai 1,2026 pamoja na Muscata nchini Oman Julai 23,2026.
Akizindua safari hiyo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza,Mkuu wa Wilaya ya Ilemela Amir Mkalipa,amesema Mkoa wa Mwanza ni wa pili katika kuchangia pato la taifa na idadi ya watu huku ukiwa ni kitovu cha mikoa ya Kanda ya Ziwa na unafikika kihurahisi hivyo usafiri wa anga ni muhimu.
Mkalipa amesema,safari hiyo itarahisisha usafiri na kuchochea uchumi kwani awali watu walikuwa wakitaka kusafiri kutoka Dodoma kuja Mwanza,iliwalazimu kuunganisha mpaka jijini Dar-es-Salaam.Huku akisisitiza kuwa safari hizi zikifanya vizuri wanaweza kushauri kuongezwa nyingine.
“Uwanja wa Mwanza ndiyo hadhi ya Kanda ya Ziwa,Rais Samia Suluhu Hassan ameruhusu Bunge kuweka bajeti ya mwaka wa fedha 2026/27 ya kujenga jengo la abiria la kimataifa “terminal” kwa sababu ni lazima uwanja huu uwe wa kimataifa,”amesema Mkalipa.
Kwa upande wake Mjumbe wa Halmashauri ya CCM Taifa (MNEC),Dkt.Angeline Mabula,amesema kwa miaka mingi,Wabunge wa Kanda ya Ziwa,walikuwa wakisisitiza umuhimu wa safari ya Mwanza-Dodoma,lakini mara nyingi ilibaki kuwa ahadi.Leo wameshuhudia utekelezaji wake rasmi, jambo ambalo limeondoa adha iliyokuwa ikiwakabili wananchi waliolazimika kupitia Dar-es-Salaam ili kufika Dodoma.
“Nawapongeza Wabunge wa Kanda ya Ziwa kwa umoja walitambua kuwa Mwanza ni kitovu cha shughuli nyingi za kiuchumi katika ukanda huu, na kuimarika kwa usafiri wa anga kati ya Mwanza na Dodoma,kutachochea maendeleo ya kiuchumi, kurahisisha shughuli za wananchi na kupunguza changamoto za usafiri zilizokuwepo hapo awali,”amesema Dkt.Angeline na kuongeza:
“Mimi pia nilikuwa mmoja wa Wabunge waliokuwa wakisisitiza umuhimu wa safari hii, na kumbukumbu za Bunge zinathibitisha juhudi hizo,”.
Mbunge wa Bariadi Vijijini Masanja Kadogosa, amesema Serikali imetekeleza ahadi ya kuanzisha safari hiyo pamoja na kuendelea na mipango ya kuupanua uwanja wa ndege wa Mwanza ili uwe na hadhi ya kimataifa.
“Tulifanya mijadala mikubwa bungeni kuhusu maendeleo ya uwanja huu, na Serikali ilitoa ahadi kwamba hatua za maboresho na upanuzi zingetekelezwa. Tayari tumeelezwa kuwa maandalizi ya ujenzi na upanuzi yanaendelea,hatua hizi zitawanufaisha wananchi wa Kanda ya Ziwa na zitafungua fursa zaidi za biashara, uwekezaji na usafiri wa kimataifa,”amesema Kadogosa.

Naye Mbunge wa Jimbo la Ilemela Kafiti William,ameomba kuongezwe siku za safari badala ya mbili ziwe tatu ili kutoa fursa zaidi kwa watu kutumia usafiri wa anga na kufanya shughuli za uchumi.


More Stories
“Serikali inathamini mchango taasisi za dini”
Kihongosi asimulia magumu aliyopitia, ni kilio na furaha
Sillo:Tanzania itakuwa mwenyeji bora AFCON 2027