June 20, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

JOWUTA yasukuma mwongozo wa kiswahili

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online

SHIRIKA la Kimataifa la Kazi Duniani (ILO) limezindua mwongozo mpya wa kusaidia wanahabari kuandika na kuripoti habari zinazohusu wahamiaji na wakimbizi kwa kuzingatia misingi ya taaluma na matumizi sahihi ya lugha.

Uzinduzi huo ulifanyika leo Juni 20, 2026, katika warsha ya viongozi wa vyama vya wafanyakazi wa sekta ya habari kutoka nchi mbalimbali za Afrika Mashariki inayoendelea mjini Mombasa, Kenya.

Akizindua mwongozo huo, Mshauri Mkuu wa Kiufundi wa ILO, Charles Autheman, amesema nyenzo hiyo imeandaliwa kusaidia wanahabari kuelewa vizuri masuala ya uhamaji na kutumia maneno yanayofaa wakati wa kuripoti habari zinazohusu wahamiaji na wakimbizi.

Autheman amesema bado kuna changamoto katika namna baadhi ya habari za uhamaji zinavyoandikwa na kutangazwa, jambo ambalo limeifanya ILO kuandaa mwongozo huo ili kutoa rejea kwa wanahabari na wadau wa sekta ya habari.

Ameeleza kuwa mwongozo huo unapatikana katika tovuti ya ILO ukiwa umetafsiriwa katika lugha mbalimbali ikiwemo Kiingereza, Kifaransa na Kiarabu, huku Kiswahili kikiwa bado hakijajumuishwa.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi katika Vyombo vya Habari Tanzania (JOWUTA), Mussa Juma, ameitaka ILO kuzingatia pia kutafsiri mwongozo huo kwa Kiswahili kutokana na ongezeko la matumizi ya lugha hiyo katika mataifa mbalimbali duniani.

Mussa amesema upatikanaji wa mwongozo huo kwa Kiswahili unaweza kusaidia wanahabari wengi zaidi katika ukanda wa Afrika Mashariki kuutumia kwa urahisi na kuongeza uelewa wa masuala ya uhakkll ni,maji.

Akijibu hoja hiyo, Autheman amesema ILO inalifanyia kazi suala hilo na kuongeza kuwa wadau wa Tanzania wanaweza pia kushiriki katika mchakato wa kutafsiri mwongozo huo. Warsha hiyo imeandaliwa na ILO kwa kushirikiana na mashirika ya wanahabari ya kikanda na imewakutanisha washiriki kutoka nchi kadhaa za Afrika Mashariki na Pembe ya Afrika.