June 19, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wahariri wahimizwa kulinda maadili ya Taifa

Na Mwandishi Wetu,Timesmajira

SEKRETARIETI ya Maadili ya Viongozi wa Umma, imewataka wahariri wa vyombo vya habari nchini kuendelea kutumia kalamu na sauti zao kama nyenzo muhimu katika kukuza maadili, uwajibikaji na uadilifu miongoni mwa viongozi wa umma.

Akisoma hotuba kwa niaba ya Jaji(Mstaafu) Sivangilwa Mwangesi ambaye ni Kamishna wa Maadili ya Umma, Katibu wa Usimamizi wa Maadili, Kassim Mkwawa katika ufunguzi wa mkutano na Wahariri wa Vyombo vya Habari uliofanyika katika Ukumbi wa PSSSF Convention Center jijini Dar es Salaam, amesema vyombo vya habari vina mchango mkubwa katika kujenga taifa lenye viongozi waadilifu na jamii inayozingatia misingi ya maadili.

Mkwawa ameeleza kuwa kwa miaka minne sasa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma imekuwa na utamaduni wa kukutana na wahariri kwa lengo la kujenga ushirikiano, kupeana elimu kuhusu Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma Na. 13 ya mwaka 1995, pamoja na kujadili namna bora ya kuimarisha maadili nchini.

Amesema ushirikiano kati ya Sekretarieti na vyombo vya habari umeleta matokeo chanya, hasa katika kusaidia taasisi hiyo kupata taarifa zinazohusu changamoto za kimaadili miongoni mwa viongozi wa umma.

“Vyombo vya habari vimekuwa msaada mkubwa sana kwetu. Kupitia habari mnazochapisha, tumekuwa tukipata taarifa zinazotusaidia kutambua changamoto mbalimbali za kimaadili na kuzifanyia kazi,” amesema.

Kwa mujibu wa hotuba hiyo, katika mwaka wa fedha 2025/26, Sekretarieti imefanya ziara katika kanda nane nchini kwa lengo la kukutana na wahariri wa kanda mbalimbali na kujadiliana kuhusu umuhimu wa ushirikiano katika kukuza maadili ya viongozi wa umma.

Amesisitiza kuwa wahariri na wanahabari ni wadau muhimu kwa sababu wana uwezo wa kukusanya, kuchakata na kusambaza taarifa kwa haraka, huku pia wakiwa na nafasi ya kuishawishi jamii kuelekea katika mwelekeo chanya.

Aidha, amewataka wahariri kujitafakari na kujiuliza mchango wao binafsi katika kukuza maadili kupitia kazi zao za kila siku.

“Ni muhimu kila mmoja wetu kujiuliza; je, tunachangia vipi kukuza uadilifu nchini? Je, tunasaidiaje kufichua vitendo vya ukiukwaji wa maadili? Hii ni kazi yetu sote,” amesisitiza.

Mkwawa ameeleza kuwa taifa lenye viongozi waadilifu hujenga mazingira bora ya maendeleo kwa kuhakikisha rasilimali za umma zinawanufaisha wananchi wote kwa usawa.

Katika wito wake kwa wahariri, amewahimiza kuendelea kuwa wazalendo na kutumia taaluma yao kujenga taifa lenye umoja, mshikamano na viongozi waadilifu.

Ameonya kuwa kukosekana kwa uadilifu kunachochea malalamiko, manung’uniko, upendeleo na mgawanyo usio sawa wa rasilimali za taifa.

Pia amepongeza vyombo vya habari nchini kwa kuendelea kufanya kazi kwa weledi na kuzingatia maadili ya taaluma yao, jambo ambalo limechangia kudumisha amani na kulinda maadili ya Kitanzania licha ya changamoto za utandawazi.

Kwa ujumla, ujumbe mkuu wa mkutano huo ulikuwa ni kusisitiza kuwa ujenzi wa taifa lenye viongozi waadilifu unahitaji ushirikiano wa karibu kati ya taasisi za umma, vyombo vya habari na jamii kwa ujumla