June 18, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kihongosi ataka Mradi wa Mgambalenga kukamilika kwa wakati

Na Agnes Alcardo, Timesmajira Online. Iringa

KATIBU wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Kenani Kihongosi, amemtaka mkandarasi anayetekeleza mradi wa umwagiliaji wa Mgambalenga uliopo katika Wilaya ya Kilolo, mkoani Iringa, kuhakikisha anakamilisha mradi huo kwa wakati ili uweze kuwanufaisha wakulima zaidi ya 1000 wanaotarajiwa kunufaika na miundombinu ya kisasa ya umwagiliaji.

Kihongosi amesema hayo leo Juni 18, 2026 wakati akiwa kwenye ziara yake ya siku nne mkoani Iringa, ambapo leo ikiwa ni siku ya kwanza. Baada ya kuwasili mkoani humo, Kihongosi alitembelea na kukagua mradi huo Mgambalenga uliopo kata ya Ruaha Mbuyuni Wilayani Kilolo mkoani Iringa na kuona maendeleo yake.

Amesema ni vyema mradi huo ukakamilika kwa wakati, kwani kukamilika kwake utanufaisha baadhi ya vijiji ikiwemo Kijiji cha Mtandika, Msosa na Ruaha Mbuyuni, huku thamani ya mradi huo ikitajwa kuwa ni Sh. Bil 23.9 ukilenga kupanua mashamba ya umwagiliaji kutoka hekta 150 hadi 1,700 ili kuongeza tija ya kilimo na kuinua uchumi wa wananchi.

“Mradi huu wa umwagiliaji Mgambalenga unatekelezwa na Tume ya Taifa ya Umwagiliaji katika Wilaya hii ya Kilolo na unatajwa kuwa miongoni mwa miradi mikubwa ya kilimo inayolenga kuongeza uzalishaji wa mazao na kuimarisha usalama wa chakula kwa wakulima,” amesema Kihongosi

Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa mradi huo Mhandisi wa Umwagiliaji Kilolo, Gerald Kapukutu, amesema mradi huo unatekelezwa na mkandarasi China Railway 15 Bureau Group Corporation kwa thamani ya Sh. Bil 23.9.

Kapukutu amesema kukamilika kwa mradi huo kutawanufaisha moja kwa moja wakulima 1,129 huku wananchi wengine wapatao 38,824 wakitarajiwa kunufaika kwa njia mbalimbali ikiwemo ongezeko la uzalishaji wa chakula na shughuli za kiuchumi.

Kwa mujibu wa Kapukutu, mawanda ya mradi yanahusisha ujenzi wa mifereji ya umwagiliaji yenye urefu wa kilomita 44.5 kwa kiwango cha zege, ujenzi wa vijengwa vya umwagiliaji, barabara za mashambani zenye urefu wa kilomita 31 pamoja na ofisi ya meneja wa mradi.

Katika kazi za awali Kapukutu amesema zimefikia asilimia 98 ya utekelezaji huku kilomita 4.4 za mifereji ya umwagiliaji zikiwa tayari zimesakafiwa kwa zege na kilomita 5.5 za barabara za mashambani zimejengwa kwa kiwango cha changarawe.

“Hadi sasa mradi umefikia asilimia 47 ya utekelezaji na unatarajiwa kukamilika Juni 27, 2027 baada ya kuongezewa muda wa utekelezaji ili kuruhusu kukamilika kwa kazi zilizobaki,” amesema Kapukutu

Hata hivyo, Kapukutu amesema mradi unakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo kuchelewa kwa malipo ya mkandarasi, mvua nyingi zilizochelewesha baadhi ya shughuli za ujenzi pamoja na uwepo wa mazao katika maeneo yaliyopangwa kupitisha mifereji ya umwagiliaji.

Changamoto nyingine ni kupanda kwa gharama za mafuta na kuongezeka kwa gharama za ajira, hali ambayo imeongeza gharama za uendeshaji wa mradi huo.

Kwa upande wake Mbunge wa Kilolo Mkoa wa Iringa, Ritta Kabati, amesema Serikali inaendelea kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa mradi huo ili kuhakikisha changamoto zilizopo zinapatiwa ufumbuzi na mradi unakamilika kwa wakati.

“Na mradi huu una nafasi kubwa ya kuleta mapinduzi ya kilimo katika Wilaya ya Kilolo kwa kuwa utawawezesha wakulima kuzalisha kwa mwaka mzima badala ya kutegemea msimu wa mvua pekee,” alisema Kabati