


Na Jouce Kasiki
Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) imesema itaendelea kuimarisha uzalishaji na usambazaji wa takwimu rasmi ili kusaidia utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, inayolenga kuifanya Tanzania kuwa na uchumi wa dola trilioni moja pamoja na kuboresha maisha ya wananchi.
Kauli hiyo imetolewa Juni 17, 2026 na Mkurugenzi wa Takwimu za Uchumi wa NBS, Daniel Masolwa, wakati wa maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayofanyika katika viwanja vya Chinangali jijini Dodoma.
Akizungumza na wananchi waliotembelea banda la NBS, Masolwa alisema taasisi hiyo inatumia maadhimisho hayo kutoa elimu kuhusu umuhimu wa takwimu rasmi katika kupanga na kutekeleza mipango ya maendeleo ya Taifa.
Alieleza kuwa kaulimbiu ya mwaka huu ya Wiki ya Utumishi wa Umma, inayosema “Kuchochea Uwajibikaji Jumuishi kwa Huduma Endelevu,” inaonesha nafasi muhimu ya takwimu katika kuongeza uwajibikaji, kufanya maamuzi sahihi na kufuatilia utekelezaji wa sera na mipango ya maendeleo.
Masolwa alisema kwa mujibu wa Sheria ya Takwimu Sura ya 351, NBS ina jukumu la kukusanya, kuchambua, kuchakata na kusambaza takwimu rasmi zinazotumiwa na serikali, sekta binafsi, watafiti na wadau mbalimbali wa maendeleo.
Alibainisha kuwa takwimu rasmi ni nyenzo muhimu katika kupanga maendeleo na kutathmini matokeo ya miradi na programu zinazotekelezwa nchini.
Miongoni mwa takwimu zinazozalishwa na NBS ni zile za mfumuko wa bei zinazotolewa kila mwezi kwa lengo la kuonesha mwenendo wa bei za bidhaa na huduma katika soko la Tanzania.
Pia, taasisi hiyo huzalisha takwimu za Pato la Taifa (GDP) kwa vipindi vya robo mwaka, ambazo hutumika kupima ukuaji wa uchumi, thamani ya uzalishaji wa bidhaa na huduma pamoja na mchango wa sekta mbalimbali katika uchumi wa nchi.
Kwa upande wa ajira, Masolwa alisema NBS hutoa taarifa zinazobainisha hali ya soko la ajira, kiwango cha ukosefu wa ajira na idadi ya wananchi wanaoshiriki katika shughuli za kiuchumi.
Aidha, NBS huzalisha takwimu za sekta za kilimo, viwanda, biashara ya kimataifa pamoja na takwimu za kijamii zinazotokana na Sensa ya Watu na Makazi, ambazo husaidia kuelewa muundo wa idadi ya watu na rasilimali watu iliyopo nchini.
Alisisitiza kuwa takwimu hizo zina mchango mkubwa katika kupima viashiria vya maendeleo ikiwemo pato la mwananchi, ukuaji wa uchumi na ustawi wa jamii.
Akizungumzia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Masolwa alisema mafanikio ya utekelezaji wake yatahitaji matumizi makubwa ya takwimu sahihi na za kuaminika katika kupanga na kufuatilia maendeleo.
Alisema dira hiyo inalenga kujenga uchumi imara, shindani na unaowanufaisha wananchi, jambo ambalo linahitaji jamii inayotegemea maarifa, ujuzi na matumizi ya takwimu katika kufanya maamuzi.
Masolwa alisema NBS itaendelea kuhakikisha takwimu rasmi zinapatikana kwa wakati, zinazingatia viwango vya ubora vinavyotakiwa kimataifa na zinachangia kwa kiasi kikubwa kufanikisha malengo ya maendeleo ya Tanzania kuelekea mwaka 2050.

More Stories
TBS kuadhimisha miaka 50,kuzindua kitabu chake
Vijana wahimizwa kutumia fursa za kiuchumi
DCP Ngoso, DCF Ngenya na DCI Mwaifuge wajionea huduma Magerezani