

Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma
AFISA Upimaji Mwandamizi wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Hussein Shambas, amemweleza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais ,Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Ridhiwani Kikwete kuhusu mfumo wa kidijitali unaoonyesha hali ya upatikanaji wa umeme katika vijiji na vitongoji mbalimbali nchini.
Aidha Waziri Kikwete amejionea Shirika hilo linavyohamasisha matumizi ya Nishati safi ya kupikia ambapo alizawadiwa jiko la umeme kidogo ili akawe balozi mzuri wa kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Akitoa maelezo mbele ya Waziri Kikwete,alipotembelea banda hilo katika maadhimosho ya wiki ya Utumishi wa Umma, Shambas alisema mfumo huo unaonyesha maeneo yote yenye umeme, yasiyo na umeme pamoja na yale yaliyo katika mpango wa kupatiwa huduma hiyo, hatua inayorahisisha upatikanaji wa taarifa kwa wananchi na wadau mbalimbali.
Aidha amesema kutokana na kasi ya utekelezaji wa miradi ya usambazaji umeme vijijini, REA imefikia asilimia 77 ya uunganishaji wa vitongoji, sawa na vitongoji 39,840 vilivyopata huduma ya umeme huku akisema kuwa vitongoji 12,736 vilivyosalia vinatarajiwa kufikiwa na huduma hiyo ifikapo mwaka wa fedha 2030/2031.
“Huu ni mfumo wa kidijitali unaowezesha wananchi kupata taarifa mbalimbali wanazozihitaji kuhusu hali ya upatikanaji wa umeme nchini mwananchi anaweza kuufikia moja kwa moja kupitia simu yake ya mkononi,” amesema Shambas.
Katika uwasilishaji wake, alimwonyesha Waziri Kikwete takwimu za Mkoa wa Pwani, Wilaya ya Bagamoyo, Jimbo la Chalinze, ambapo mfumo huo ulionyesha kuwa vitongoji 286 tayari vina huduma ya umeme, vitongoji 133 vipo katika mpango wa kuunganishiwa umeme, huku vitongoji 50 vikiwa katika hatua ya utekelezaji ambapo wakandarasi wanaendelea na kazi maeneo husika.
Alifafanua kuwa mfumo huo una uwezo wa kuonyesha taarifa kwa undani hadi ngazi ya kitongoji, ikiwemo vitongoji vilivyopata umeme na vile vilivyopo katika mipango ya utekelezaji.
Kwa mfano, alimwonyesha Waziri taarifa za Kijiji cha Msoga na vitongoji vyake ambavyo tayari vimeunganishiwa umeme na ambavyo bado javijaunganishwa na huduma hiyo.
Katika hatua nyingine inayolenga kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia, Waziri Kikwete alikabidhiwa jiko la umeme la plate mbili ili awe balozi na mfano wa matumizi ya nishati safi katika maeneo mbalimbali nchini.

More Stories
DCP Ngoso, DCF Ngenya na DCI Mwaifuge wajionea huduma Magerezani
VETA yathibitisha uwezo kwa mhitimu mlemavu
TANTRADE yafungua fursa za Biashara kati ya Tanzania,Urusi