June 17, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mwaselela ataka kudumishwa kwa amani na mshikamano

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online, Mbeya

MJUMBE wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (MNEC),Ndele Mwaselela, amewataka viongozi wa dini na vyama vya siasa kutumia majukwaa yao kuhubiri amani, upendo na mshikamano, pamoja na kumwombea Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Samia Suluhu Hassan, ili nchi iendelee kuwa na utulivu.

Mwaselela alitoa wito huo Juni 16, 2026, wakati akitoa salamu za Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika ibada ya mazishi ya shangazi wa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mbeya na Mbunge wa Jimbo la Mbeya Mjini,Patrick Mwalunenge iliyofanyika katika Kata ya Ilima, Wilaya ya Rungwe .

Akizungumza katika ibada hiyo, Mwaselela amesema CCM inaendelea kuthamini umoja, upendo na amani kama nguzo muhimu za maendeleo ya taifa.

“Sisi tunapenda sana umoja na amani. Maandiko matakatifu yanatufundisha kuhusu amani na upendo. Upendo hauna majivuno wala jeuri, na ndiyo msingi unaotukutanisha leo,” amesema Mnec.

Alisema mkusanyiko huo umeonyesha umuhimu wa mshikamano na amani iliyopo nchini, akibainisha kuwa utulivu huo unatokana na uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, ambaye pia ni Amiri Jeshi Mkuu.

“Tunapotoka sehemu mbalimbali na kufika hapa salama ni kwa sababu ya amani iliyopo nchini. Hivyo ninaomba viongozi wa dini na wa vyama vya siasa wanaposimama kwenye majukwaa yao waendelee kuombea amani, upendo na Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan,” alisema Mwaselela.

Mwaselela alisisitiza kuwa umoja na utulivu vinapaswa kuwa vipaumbele vya kwanza kwa Watanzania kwa kuwa bila amani shughuli za uzalishaji, biashara na maendeleo haziwezi kufanyika kwa ufanisi.

“Bila umoja huwezi kulima, huwezi kufanya biashara wala mikusanyiko ya kijamii. Viongozi wa dini na vyama vya siasa wanapaswa kuwa mabalozi wa amani kila mahali na kuhakikisha hakuna chokochoko zinazoweza kuhatarisha utulivu wa nchi,” aliongeza.

Katika ibada hiyo, viongozi kutoka vyama mbalimbali vya siasa, ikiwemo Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), walihudhuria na kushiriki shughuli za mazishi.

Akizungumza kwa niaba ya wananchi waliohudhuria, Tumani Atupakusye alisema amani iliyopo nchini ni tunu muhimu inayopaswa kulindwa na kila Mtanzania.

“Amani tuliyonayo ni ya thamani kubwa. Tunapaswa kuitunza na kuhakikisha umoja na mshikamano vinaendelea kudumishwa kwa manufaa ya taifa letu,” alisema.