Na Fresha Kinasa,TimesMajira Online, Mara.
JAMII imehimizwa kuweka mkazo katika kuwalea watoto kwa kuzingatia malezi bora na maadili mema na kuhakikisha wanapata haki zao za msingi, hususan elimu, ili waweze kufikia malengo yao kimaisha.
Wito huo umetolewa Juni 16, 2026, na Mkurugenzi wa Shirika la Hope for Girls and Women in Tanzania, linalojishughulisha na mapambano ya ukatili wa kijinsia Mkoa wa Mara Rhobi Samwelly, wakati wa kilele cha maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika yaliyofanyika katika Kituo cha Nyumba Salama cha Kiabakari kinachomilikiwa na Shirika hilo, Wilaya ya Butiama.
Ambapo, kauli mbiu kwa mwaka huu inasema, ‘Mtoto ni Malezi Msingi wa Familia Bora kwa Taifa Imara’
Maadhimisho hayo yamewakutanisha viongozi wa serikali, wananchi pamoja na wadau mbalimbali wa maendeleo. Ambapo Rhobi amesema, malezi yanayozingatia maadili mema ni msingi muhimu wa kujenga kizazi chenye nidhamu, heshima na uwajibikaji katika jamii.

Amesisitiza, wazazi, walezi na jamii kwa ujumla wanapaswa kushirikiana kuhakikisha watoto wanalelewa katika mazingira salama yatakayowajengea uwezo wa kutambua mema na mabaya.
“Utoaji wa haki za msingi kwa watoto, hususan elimu, ni nguzo muhimu katika kufanikisha ndoto zao na kuwawezesha kufikia malengo waliyojiwekea maishani. Elimu huwapa watoto maarifa, ujuzi na kujiamini. Hivyo, jamii inapaswa kuendelea kuweka mazingira rafiki yatakayowahamasisha watoto wote kupata fursa sawa za kujifunza bila ubaguzi wa aina yoyote,” amesema Rhobi.
Pia, amewahimiza wadau mbalimbali, viongozi wa serikali na wananchi kuendelea kushirikiana katika kulinda haki za watoto na kuhakikisha wanalelewa katika mazingira yanayoheshimu utu wao na kuwapa matumaini ya maisha bora ya baadaye.
Afisa Ustawi wa Jamii wa Wilaya ya Butiama, Abel Ginchaine, ameitaka jamii kuimarisha ulinzi na usalama wa watoto pamoja na kupinga vitendo na mila kandamizi zinazohatarisha ustawi na maendeleo yao. Huku akiswma jukumu la kumlinda mtoto ni la kila mwanajamii, hivyo ushirikiano unahitajika ili kuhakikisha watoto wanakua katika mazingira salama.


More Stories
Taasisi zahimizwa kuimarisha uwajibikaji kwa jamii
NMB yazindua Super App,elimu ya fedha yapewa kipaumbele
AGL Tanzania yatekeleza Mpango wa “Plastic-Less” kwa Kulinda Mazingira