June 16, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mwanza wataka suluhu ya kudumu ya maji

*Aweso amsimamisha kazi Meneja usambazaji maji,aahidi maboresho

Judith Ferdinand, Mwanza

Baadhi ya wananchi wa Jiji la Mwanza wameitaka Serikali kutafuta suluhisho la kudumu la changamoto ya upatikanaji wa maji ambayo imeendelea kwa zaidi ya wiki mbili, licha ya hatua mbalimbali zinazochukuliwa kurejesha huduma hiyo.

Wakizungumza na Majira Juni 16, 2026, wananchi hao wamesema hatua za kinidhamu zinazochukuliwa dhidi ya kiongozi wa mamlaka husika ni muhimu, lakini haziwezi kuwa suluhisho la kudumu kwa tatizo la maji linalowaathiri wakazi wa jiji hilo.

Mmoja wa wananchi hao, Elizabeth Kalonga, amesema Serikali inapaswa kuweka mkakati madhubuti wa kuhakikisha huduma ya maji haiathiriki pale panapotokea hitilafu katika mitambo ya kusukuma maji au changamoto za umeme.

“Tumemsikia Waziri wa Maji amemsimamisha kazi mmoja wa viongozi wa Mamlaka ya Maji, lakini hilo pekee si suluhisho. Kinachohitajika ni kuwa na mfumo wa dharura au mitambo mbadala itakayowezesha huduma ya maji kuendelea hata pale kunapotokea hitilafu za kiufundi au changamoto za umeme,”amesema Kalonga.

Amos Shawishi,amesema Serikali ifanye suala la maji kuwa kipaumbele kwa kuweka mifumo ya maji ya kudumu kwa kuwa na uwiano sawa la ongezeko la watu na miundombinu inayotoa huduma.

“Changamoto kwenye mitambo ni kawaida, lakini kukiwa na miundombinu ambayo ina nguvu kubwa kuliko mahitaji ya watu ina maana kutakuwa na maji ya ziada.Hivyo likitokea tatizo la umeme au mitambo kama hivi sasa haita athiri sana kwani watu wataendelea kupata huduma kwa sababu yatakuwepo maji ya ziada wakati huo ufumbuzi wa tatizo ukiendelea,”alisema Shawishi.

Kwa upande wake Josephine Mdeme,amesema Serikali inapaswa kuweka watu wanaowajibika wakati wote na kuchukua hatua za haraka pindi inapotokea changamoto ambayo inaweza kusababisha ukosefu wa maji kwa wananchi.

Amesema maji ni uhai,yanapokosekana inakuwa changamoto katika jamii kwanza kiafya na hata kiuchumi,ambapo alitolea mfano katika kipindi hiki ambacho Jiji la Mwanza limekumbwa na kero ya ukosefu wa maji alilazimika kununua ndoo 10 za lita 20,kwa sh.10,000 wakati kiasi hicho mara nyingi ndicho utumika kulipia ankara ya maji kwa mwezi mzima.

Itakumbukwa kuwa Juni 15,2026 Waziri wa Maji, Jumaa Aweso,alimsimamisha kazi Meneja wa Uzalishaji na Usambazaji wa Maji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA), Mhandisi Ramadhani Mramba, kwa kile kilichoelezwa kuwa ni kushindwa kusimamia ipasavyo huduma ya usambazaji maji kwa wakazi wa Jiji la Mwanza.

Aweso amechukua hatua hiyo baada ya kufanya ziara ya kukagua vyanzo vya maji Capripoint na Butimba ili kujionea hali halisi ya upatikanaji wa maji katika jijini humo,ikiwa ni maelekezo ya Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, baada ya Serikali kupokea malalamiko ya wananchi kuhusu uhaba wa maji uliodumu kwa zaidi ya wiki mbili kwa baadhi ya maeneo ya Jiji la Mwanza.

Ambapo amesema,uamuzi huo umechukuliwa kwa lengo la kuimarisha ufanisi wa utoaji wa huduma ya maji baada ya kubaini changamoto za kiutendaji wakati wa ziara yake katika maeneo mbalimbali, ikiwemo Kata za Buhongwa na Mecco, Wilaya Nyamagana na Ilemela mkoani Mwanza.

Ameeeleza kutoridhishwa na hali ya upatikanaji wa maji katika Kata ya Mecco, ambapo wananchi wamekuwa wakilalamikia ukosefu wa huduma hiyo kwa muda mrefu.

Akizungumza na wananchi wa Buhongwa, Butimba na Mecco,Aweso amesema Serikali imejipanga kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji safi na salama kwa uhakika, huku akiahidi kuwa changamoto hiyo haitajirudia.

Hata hivyo mahitaji ya maji jijini Mwanza kwa siku ni takribani lita milioni 172, uwezo wa uzalishaji maji kwa sasa uliopo kwa siku ni lita milioni 138 kupitia vyanzo viwili vya maji.Ambapo chanzo cha Capripoint kina uwezo wa kuzalisha lita za milioni 90 kwa siku huku Butimba kikizalisha lita milioni 48 kwa siku hivyo kuwa na upungufu wa lita milioni 34 kwa siku.
Mwisho