June 15, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TASHICO,LMC waingia makubaliano usafirishaji majini

Na Judith Ferdinand, Timesmajira Online- Mwanza

USAFIRISHAJI wa mizigo na abiria kupitia Ziwa Tanganyika inatarajia kupata msukumo mpya baada ya nchi ya Tanzania  na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo(DRC),kuingia makubaliano ya ushirikiano kwa miaka mitatu.

Makubaliano hayo ambayo yameanza kutekelezwa baada ya kutiwa saini leo  Juni 15,2026 kati ya Kampuni ya Meli Tanzania(TASHICO) na Kampuni ya Taifa ya Meli ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Lignes Maritimes Congolaises, LMC),yanayolenga  kuimarisha biashara ya kikanda, kuongeza ufanisi wa usafirishaji na kupanua fursa za kiuchumi kwa nchi hizo mbili.

Huku yakihusisha ushirikiano katika kukuza usafiri kwa njia ya maji, kuboresha huduma za usafirishaji wa shehena na abiria pamoja na kubadilishana utaalamu na uzoefu katika sekta ya ubaharia kati ya kampuni hizo mbili.

Akizungumza wakati wa hafla ya utiaji saini, Mkurugenzi Mtendaji wa TASHICO, Eric Hamissi amesema kupitia ushirikiano huo, Tanzania itanufaika kwa kupanua soko la huduma za usafirishaji, huku ikiimarisha nafasi yake kama lango la biashara kwa nchi za Afrika ya Mashariki na Kati hususani DRC.

Hamissi amesema,makubaliano hayo  yatawezesha kubadilishana utaalamu kati ya pande hizo mbili, ambapo LMC ina uzoefu mkubwa wa usafiri wa baharini kupitia Bahari ya Atlantiki, huku Tanzania ikiwa na uzoefu katika usafiri wa maziwa makuu.

Amesema kwa kuanzia, kampuni hizo zinatarajia kuanza na matumizi ya meli za kukodi ili kukidhi mahitaji ya soko, huku mipango ya muda mrefu ikiwa ni kujenga na kumiliki meli za pamoja zitakazohudumia biashara katika ukanda huo.

Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa LMC, Frank  Nkulu,amesema kutiwa saini kwa makubaliano hayo ni hatua muhimu katika kuimarisha uhusiano wa kiuchumi na kibiashara kati ya Tanzania na DRC,ambao unalenga kujenga mfumo wa kisasa na wenye ufanisi wa usafirishaji utakaokidhi mahitaji ya wafanyabiashara na jamii zinazozunguka Ziwa Tanganyika.

Makubaliano hayo pia yanatarajiwa kuimarisha matumizi ya Ziwa Tanganyika kama njia muhimu ya usafirishaji na hivyo kufungua fursa za biashara kwa nchi jirani ikiwemo Zambia na Burundi.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TASHICO,Meja Jenerali Mstaafu John Mbunge,amesema makubaliano hayo yataisaidia Congo kupunguza utegemezi wa usafirishaji wa mizigo kupitia Bahari ya Atlantiki na badala yake kuimarisha matumizi ya njia ya Bahari ya Hindi kupitia Tanzania.

Amesema hatua hiyo itaziwezesha kampuni hizo kufikia masoko ya dunia kupitia bandari za Tanzania, huku zikichangia kuongeza ushindani wa huduma za usafirishaji.

Muwakilishi wa Katibu Mkuu Wizara ya Uchukuzi, Manchali Suguta amesema Serikali imekuwa ikiwekeza fedha nyingi kwenye suala la usafirishaji wa mizigo na abiria ili kukuza biashara huku makubaliano hayo yanalenga kukuza ajira na vipato vya watu wao.

Hata hivyo makubaliano hayo yanakuja wakati Bandari ya Dar-es-Salaam inaendelea kuimarisha nafasi yake katika kuhudumia mizigo ya nchi jirani huku takwimu zinaonesha kuwa sehemu kubwa ya mizigo ya DRC hupitia Tanzania, jambo linaloifanya nchi kuwa kitovu muhimu cha usafirishaji katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.