Na Zena Mohamed,TimesmajiraOline,Dodoma
IMEELEZWA kuwa Tanzania ina uwezo mkubwa wa kuzalisha bidhaa bora za ngozi zinazoweza kushindana katika soko la kikanda na kimataifa kutokana na upatikanaji wa malighafi za kutosha na uwekezaji uliofanywa katika sekta hiyo.
Hayo yamesemwa bungeni jijini hapa leo Juni 15,2026 na Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii wa Watumishi wa Umma (PSSSF) Fortunatus Magambo wakati akiwasilisha taarifa shughuli na mafanikio ya Kiwanda cha Ngozi cha Kilimanjaro (Kilimanjaro International Leather Industries Company Limited-KLICL).
Amesema KLICL, imeendelea kuwa miongoni mwa viwanda vikubwa vya uchakataji wa ngozi nchini kwa kuzalisha bidhaa mbalimbali zikiwemo viatu, mikanda, mabegi na bidhaa nyingine zinazokidhi viwango vya ubora vya kimataifa.
Kutokana na ubora wa bidhaa zinazozalishwa na Kiwanda hicho Magambo amewataka wabunge kuwa mabalozi wa bidhaa za ngozi zinazozalishwa nchini kwa kuzitumia na kuzitangaza, hatua itakayosaidia kukuza viwanda vya ndani, kuongeza ajira na kuimarisha uchumi wa taifa.
“Tunawaomba Waheshimiwa Wabunge muwe mabalozi wa bidhaa za ngozi zinazozalishwa hapa nchini. Mkitumia na kuzitangaza, mtasaidia kujenga imani kwa wananchi na kuongeza soko la bidhaa zetu za ndani,” amesema Magambo.
Aidha Magambo amesema kuwa kiwanda hicho kinaendelea kutekeleza mkakati wa kupanua masoko yake ndani na nje ya nchi ili kuhakikisha uwezo mkubwa wa uzalishaji uliowekezwa unatumika kikamilifu. Alitaja masoko yanayolengwa kuwa ni pamoja na nchi za Afrika Mashariki na mataifa mengine kama China, Saudi Arabia, Italia, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), Misri, Pakistan na Uturuki.
Vilevile ameeleza kuwa matumizi makubwa ya bidhaa zinazozalishwa nchini yatasaidia kuongeza thamani ya mazao ya mifugo, kuchochea ukuaji wa sekta ya viwanda, kuongeza ajira kwa vijana na kuimarisha mapato ya fedha za kigeni kupitia mauzo ya bidhaa hizo nje ya nchi.
Hata hivyo Magambo amesema kuwa kuwa Kiwanda hicho kimefanikiwa kuuza vipande 48 vya ngozi ya mbuzi kwenda China kwa thamani ya Dola za Marekani 15,000, hatua inayotajwa kuwa ishara ya kuimarika kwa mahitaji ya bidhaa za ngozi zinazozalishwa nchini katika masoko ya kimataifa.
Pamoja na mafanikio hayo, Magambo ametaja changamoto kubwa iliyopo kwa sasa ni upanuzi wa masoko ili kuendana na uwezo wa uzalishaji wa kiwanda hicho, akisisitiza kuwa ushirikiano wa viongozi, sekta binafsi na wananchi katika kuhamasisha matumizi ya bidhaa za ndani ni muhimu katika kufanikisha azma ya Tanzania ya kujenga uchumi wa viwanda.


More Stories
TASHICO,LMC waingia makubaliano usafirishaji majini
Wataalamu wa Maendeleo kukutana Mwanza kwa siku tatu
Wasomi wahimizwa kuelimisha jamii na kulinda Taswira