June 11, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Airtel Afrika yachapisha ripoti ya Maendeleo 2026

Na Mwandishi wetu,Timesmajira

Kampuni ya Airtel Africa Plc, mtoa huduma wa mawasiliano na huduma za kifedha kwa njia ya simu katika nchi 14 za Afrika ikiwemo Tanzania, imechapisha Ripoti yake ya Maendeleo ya mwaka 2026 ikibainisha mafanikio makubwa yaliyopatikana katika kupanua huduma za mawasiliano, kuimarisha ujumuishaji wa kifedha na kuchangia maendeleo endelevu ya jamii katika mwaka wa fedha 2025/26.

Ripoti hiyo inaonesha kuwa kampuni imeendelea kuwekeza katika miundombinu ya kidijitali, huduma za fedha kwa njia ya simu pamoja na ushirikiano wa kimkakati unaolenga kuboresha maisha ya wananchi na kufungua fursa za kiuchumi katika maeneo mbalimbali ya Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara.

Akizungumzia mafanikio hayo, Mtendaji Mkuu wa Airtel Africa, Sunil Taldar, alisema upatikanaji wa mawasiliano, huduma za kifedha na elimu ya kidijitali unaendelea kuwa nyenzo muhimu katika kukuza uchumi wa bara la Afrika.

Alisema kampuni imeendelea kupanua mtandao wake, kuongeza matumizi ya simu janja na kuimarisha huduma za Airtel Money ili kuwafikia wananchi wengi zaidi, hususan wanaoishi katika maeneo ya vijijini na ambayo bado hayajafikiwa kikamilifu na huduma za kidijitali.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, watu wanaofikiwa na huduma za mtandao wa simu wameongezeka na kufikia asilimia 81.9 mwaka 2025/26 kutoka asilimia 81.2 mwaka uliotangulia. Aidha, upatikanaji wa huduma za intaneti katika maeneo ya vijijini umeongezeka hadi asilimia 73.1 kutoka asilimia 72.2.

Ripoti hiyo pia inaonesha kuwa matumizi ya simu janja yameongezeka hadi asilimia 49.5 kutoka asilimia 44.8 mwaka uliopita, huku idadi ya wateja wanaotumia huduma za data ikifikia asilimia 45.9 kutoka asilimia 44.2.

Katika eneo la huduma za kidijitali, thamani ya miamala iliyofanyika kupitia programu ya My Airtel ilifikia dola za Marekani bilioni 8.3, ikiwa ni ongezeko la asilimia 80 ikilinganishwa na mwaka uliopita. Watumiaji hai wa kila mwezi wa programu hiyo walifikia milioni 10.5.

Kwa upande wa ujumuishaji wa kifedha, Airtel Africa imeendelea kupanua huduma za Airtel Money ambapo idadi ya wateja imeongezeka kutoka milioni 44.6 mwaka 2024/25 hadi zaidi ya milioni 54 mwaka 2025/26. Takribani asilimia 44.1 ya wateja hao ni wanawake.

Thamani ya miamala iliyochakatwa kupitia Airtel Money imefikia dola za Marekani bilioni 196 kutoka dola bilioni 136 mwaka uliopita, jambo linaloonesha kuongezeka kwa matumizi ya huduma za kifedha za kidijitali katika nchi zinazohudumiwa na kampuni hiyo.

Katika jitihada za kuchangia maendeleo ya kijamii na kiuchumi, mtandao wa mawakala wa Airtel Money umeongezeka hadi mawakala milioni 2.4 kutoka milioni 1.7 mwaka uliotangulia, hatua inayochangia kuongezeka kwa fursa za ajira na ujasiriamali.

Aidha, uwiano wa wanawake katika nguvu kazi ya Airtel Africa umeongezeka hadi asilimia 29.9 kutoka asilimia 29.2 mwaka uliopita.

Katika sekta ya elimu, ushirikiano kati ya Airtel Africa Foundation na UNICEF umewezesha shule 3,043 kuunganishwa na huduma za intaneti bila malipo kufikia Machi 31, 2026, kutoka shule 2,176 mwaka 2024/25.

Kwa upande wa mazingira, kampuni imeendelea kuchukua hatua za kupunguza athari za shughuli zake kwa mazingira kwa kuongeza matumizi ya nishati safi. Zaidi ya maeneo 950 ya miundombinu ya kampuni yalihamishwa kutoka matumizi ya nishati isiyounganishwa na gridi ya taifa kwenda kwenye umeme wa gridi ya taifa, ikilinganishwa na maeneo 500 mwaka uliopita.

Hatua hiyo imechangia kupunguza matumizi ya dizeli kwa lita milioni 9.1 ndani ya mwaka mmoja. Vilevile, asilimia 94 ya taka zote zilizozalishwa na kampuni zilirejelewa, kutoka asilimia 93 mwaka uliotangulia.

Ripoti ya Maendeleo ya Airtel Africa ya mwaka 2026 imeandaliwa kwa kuzingatia viwango vya kimataifa vya Global Reporting Initiative (GRI) pamoja na miongozo ya sekta ya mawasiliano ya simu ya GSMA.

Kwa sasa, Airtel Africa inahudumia zaidi ya wateja milioni 183.5 katika nchi 14 za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, huku ikiendelea kutekeleza dhamira yake ya kuendeleza ujumuishaji wa kidijitali na kifedha kwa wananchi kupitia huduma za mawasiliano na teknolojia.