June 11, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Aomba kujengewa nyumba,usafiri kwa mjukuu mwenye ulemavu

Na Judith Ferdinand, Timesmajira Online- Mwanza

MKAZI wa Nyasaka B, Kata ya Kawekamo wilayani Ilemela mkoani Mwanza, Debora Manyama maarufu kama Bibi Ayub, mwenye umri wa miaka 60, ameomba msaada wa kujengewa nyumba pamoja na kupatiwa usafiri wa kumpeleka na kumrudisha mjukuu wake, Ayubu Jackson (14), anayesoma darasa la nne katika Kituo cha Elimu ya Mahitaji Maalumu Huruma.

Manyama ameomba msaada huo hivi karibuni wakati akizungumza na Majira,mara baada ya Mkurugenzi wa Taasisi ya Mwanangu Development Tanzania(MWADETA), Walter Miya,kumtembelea bibi huyo nyumbani kwake,ili kujionea mazingira wanayoishi na mjukuu wake.

Manyama amesema, amekuwa mlezi wa Ayubu tangu akiwa na umri wa miaka mitano baada ya kukataliwa na ndugu wa upande wa baba kutokana na changamoto ya kifafa aliyokuwa nayo. Alieleza kuwa mtoto huyo aliletwa akiwa katika hali mbaya kiafya,amechubuka mwili mzima na baadaye mama yake kutoweka baada ya kuhojiwa na madaktari kuhusu chanzo cha matatizo yake.

Kwa mujibu wa Manyama, alikaa na Ayubu kwa miezi mitatu katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando kabla ya hospitali hiyo kuendelea kumhudumia kwa miezi sita kutokana na matatizo ya kifua kikuu (TB), kifafa na majeraha aliyokuwa nayo. Baada ya kupata nafuu, alipelekwa katika kituo maalumu cha malezi na baadaye kupata nafasi ya masomo.

Amesema kwa miaka kadhaa wadau mbalimbali walimsaidia Ayubu katika masuala ya elimu na matibabu, lakini kwa sasa amebaki na jukumu la kumlea huku akikabiliwa na changamoto nyingi za kiuchumi na kifamilia,ambapo anaishi na pia wagonjwa wengine wawili, akiwemo mdogo wake aliyepooza pamoja na mume wake ambaye ni mgonjwa wa pumu.

Akizungumzia changamoto kubwa inayomkabili kwa sasa, Debora alisema analazimika kutembea kwa takribani saa moja kumpeleka Ayubu shuleni na saa nyingine moja kumrudisha nyumbani kila siku. Alisema hali hiyo inapunguza muda wa kujishughulisha na biashara ndogo ndogo zinazomuingizia kipato cha familia.

Pia amesema nyumba anayoishi imebomoka upande mmoja,ambapo mazingira ya makazi hayo ni hatari kwa Ayubu ambaye mara kadhaa amekuwa akianguka kutokana na changamoto ya kifafa. Kwa mujibu wake, aliwahi kupata jeraha karibu na jicho baada ya kuangukia jiwe, jambo lililohitaji matibabu ya haraka katika kituo cha afya.

“Naiomba Serikali, taasisi na wasamaria wema kunisaidia kwa kunijengea nyumba salama na kupatiwa usafiri ili kumwezesha mjukuu wangu kuendelea na masomo katika mazingira bora na yenye usalama,huku nikipata muda wa kutafuta riziki,”amesema Manyama.

Kwa upande wa kipato, Debora amesema hutegemea biashara ndogo ya kuuza mayai na mbogamboga, lakini mapato yake ni madogo na yasiyotabirika. Wakati mwingine hupata faida ya kati ya sh.1,000 hadi sh.3,000 kwa siku, kiasi ambacho hakitoshelezi mahitaji ya chakula, dawa na huduma nyingine muhimu kwa familia.

Mkurugenzi wa Taasisi ya Mwanangu Development Tanzania (MWADETA), Walter Miya,amesema taasisi hiyo imekuwa ikifuatilia watoto wenye mahitaji maalumu wanaosoma katika Kituo cha Elimu Maalumu Huruma kwa lengo la kubaini changamoto wanazokabiliana nazo na kushirikiana na wadau pamoja na Serikali katika kutafuta suluhisho.Familia ya Ayubu ni miongoni mwa familia 10,walizozibaini kuwa zinahitaji msaada wa karibu zaidi.

Kwa upande wake, Ofisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Mwanza, Baraka Makona,amesema mwaka 2017 Serikali ilitoa muongozo wa ushughulikiaji wa watoto walio katika mazingira hatarishi kwa kuwatambua wote,huku mwaka 2022 ilianzisha bajeti maalumu kwa ajili ya huduma za ustawi wa jamii,ambapo kuna maeneo 13 na eneo moja wapo la kipaumbele ni huduma kwa watu wenye ulemavu wakiwepo watoto.

Amesema kuna baadhi ya maeneo licha ya uwepo wa Maofisa Ustawi wa Kata lakini bado watoto hawapati huduma na kuendelea kufungiwa ndani,hivyo mkakati uliopo kama Mkoa ili kuhakikisha watoto wote wanafikiwa ni kuwasajili.

“Ofisi ya Waziri Mkuu imekuwa ikituongoza kwenye jambo hili la mfumo maalumu wa kuwasajili watu wote wenye ulemavu wakiwemo watoto.
Mwanza tumeanza takribani mwezi mmoja sasa,kufanya usajili kwa kutumia simu zetu za mkononi kuna programu maalumu ambao wanatumia Maofisa Ustawi wa Jamii pamoja na watu wa TEHAMA,”amesema Makona.

       Mwisho