Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika Awamu ya Pili ya Majadiliano ya Biashara na Uwekezaji kati ya Sekta Binafsi na Serikali kwa mwaka 2026 .
Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mkutano huo, Afisa Mtendaji Mkuu wa Chemba ya Taifa ya Biashara (TNCC), Oscar Kissanga, amesema majadiliano hayo yatafanyika Juni 30, 2026 jijini Dar es Salaam
Amesema zaidi ya wafanyabiashara, wawekezaji na wadau 400 kutoka sekta binafsi na serikali wanatarajiwa kushiriki katika kongamano hilo lenye lengo la kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali na Sekta Binafsi.
“Lengo kuu la mkutano huu ni kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali na Sekta Binafsi kupitia majadiliano ya fursa, changamoto na suluhisho za kukuza uchumi na mazingira bora ya biashara nchini,” amesema Kissanga.
Ameeleza kuwa kongamano hilo ni mwendelezo wa majadiliano ya kwanza yaliyofanyika Desemba 2024, yaliyowakutanisha wadau wa sekta binafsi na serikali kujadili masuala mbalimbali yanayohusu biashara na uwekezaji nchini.
Kissanga amesema mbali na uwepo wa Waziri Mkuu kama mgeni rasmi, kongamano hilo litawakutanisha viongozi wa serikali, taasisi za kifedha, washirika wa maendeleo na wadau wengine wa uchumi watakaoshiriki mijadala mbalimbali ya kisera na kiuchumi.
Aidha, amesema kongamano hilo litashuhudia uzinduzi wa Katiba Iliyoboreshwa ya TNCC, Mpango Mkakati wa TNCC wa miaka ijayo pamoja na mfumo wa kidijitali wa Tanzania Chamber Portal (TCP), utakaorahisisha upatikanaji wa huduma kwa wanachama wa chemba hiyo. Pia kutakuwa na utiaji saini wa hati mbalimbali za makubaliano (MoUs) kati ya wadau wa biashara na uwekezaji.
Kissanga ametoa wito kwa wafanyabiashara, taasisi za sekta binafsi, viongozi wa serikali na wadau wa maendeleo kushiriki kikamilifu katika kongamano hilo, akisisitiza kuwa ni jukwaa muhimu la kuhakikisha sauti ya sekta binafsi inasikika katika mchakato wa kutunga sera na kufanya maamuzi yanayolenga kuchochea biashara, uwekezaji na ukuaji wa uchumi wa Tanzania.
Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha TEHAMA wa TNCC, Florian Mihyo, amesema mfumo wa TCP umeundwa kuunganisha huduma zote muhimu za TNCC katika jukwaa moja la kidijitali.
“Mfumo huu utawawezesha wanachama kujisajili, kufanya malipo, kupata vyeti na nyaraka za biashara, pamoja na kufuatilia taarifa za mafunzo, matukio na fursa mbalimbali za biashara kwa urahisi zaidi,” amesema Mihyo.
Ameongeza kuwa mfumo huo umejengwa kwa kuzingatia viwango vya kisasa vya usalama wa taarifa na utasaidia kuongeza ufanisi, uwazi na ushirikishwaji wa wanachama wa TNCC ndani na nje ya Tanzania huku ukipunguza urasimu katika utoaji wa huduma.

More Stories
Historia ya Uhuru wa Tanzania na ukombozi wa Afrika kung’ara Paris
CBE yawashirikisha Wadau kuboresha mitaala Tisa ya masomo
Mwaselela aahidi kumtetea Rais Samia