June 11, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mapato ya Ndani yaimarisha Bajeti ya Serikali

Na Joyce Kasiki, Dodoma

WAZIRI  wa Fedha  Balozi Khamis Mussa Omar  amesema Serikali imepata mafanikio makubwa katika utekelezaji wa Bajeti ya mwaka 2025/2026 kutokana na ukusanyaji mzuri wa mapato ya ndani yaliyofikia malengo yaliyowekwa, hali iliyowezesha kuendelea kutekeleza majukumu mbalimbali ya maendeleo na huduma kwa wananchi.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma leo Juni 10, 2026 kuhusu utekelezaji wa bajeti na mwelekeo wa bajeti ijayo, Waziri huyo alisema pamoja na mafanikio hayo, mwaka 2025/2026 ulikuwa na mahitaji na changamoto maalumu katika upande wa matumizi ya Serikali, ambazo zitafafanuliwa kwa kina katika tathmini rasmi ya utekelezaji wa bajeti hiyo.

Alieleza kuwa mafanikio ya ukusanyaji wa mapato ya ndani yameendelea kuimarisha uwezo wa Serikali wa kugharamia shughuli zake za maendeleo na matumizi ya kawaida bila kutegemea kwa kiwango kikubwa vyanzo vya nje.

Kwa mujibu wa Waziri huyo, sehemu kubwa ya fedha za maendeleo katika.mwaka ujao wa fedha, itaelekezwa katika kuendeleza miradi ya kimkakati ikiwemo ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR), upanuzi na uboreshaji wa mtandao wa barabara nchini, uwekezaji katika miradi ya maji, maendeleo ya sekta ya nishati pamoja na ujenzi wa rasilimali watu na ujuzi.

Alisema Serikali itaendelea kuhakikisha miradi hiyo inatekelezwa kwa ufanisi ili kuchochea ukuaji wa uchumi, kuongeza ajira na kuboresha huduma za kijamii kwa wananchi.

Aidha, alisisitiza kuwa usimamizi madhubuti wa mapato na matumizi ya Serikali utaendelea kuwa nguzo muhimu katika kufanikisha malengo ya maendeleo yaliyowekwa kwa mwaka wa fedha 2026/2027.