June 5, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

CCM yakemea vitendo vya ubakaji,ulawiti,ushoga

Na Agnes Alcardo, Timesmajira Online,-Arusha

KATIBU wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Kenani Kihongosi, ametoa wito kwa wazazi na jamii kwa ujumla kuwalinda watoto wao dhidi ya vitendo vya kikatili ikiwemo ubakaji na ulawiti.

Kihongosi ametoa wito huo Juni 5, 2026 wakati akizungumza na wananchi na wanachama wa CCM wa Shina Namba Saba, Tawi la Moivo,wilayani Arumeru mkoani Arusha, ikiwa ni siku ya pili ya ziara yake mkoni humo.

Kihongosi, ametoa wito huo baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa wakazi wa Kata ya Moivo, wilayani humo, wakidai kuwa watoto wao wamekuwa wakibakwa na wengine kulawitiwa, huku wanaofanya vitendo hivyo wakiachwa huru uraiani licha ya kuwafikisha katika vyombo vya sheria.

“Mheshimiwa wakazi wa hapa tunachangamoto kubwa tunaomba mtusaidie, watoto wetu wanafanyiwa vitendo vya kikatili wanabakwa na kulawitiwa, chakushangaza wanaowafanyia vitendo hivyo tukiwaripoti polisi baada ya muda tunawaona tena mtaani.

Suala hili limekuwa likituumiza sana, kwani watoto wetu ni wadogo chini ya miaka 18. Tunaomba Serikali iingilie kati,” amesema mmoja wa wakazi wa eneo hilo.

Pia, mkazi mwingine alilalamikia suala la vijana wengi katika eneo lao kujihusisha na vitendo vya uvutaji bangi, akisema kuwa hali hiyo imekuwa ikihatarisha jamii nzima.

Kihongosi, amesema Serikali na CCM imekuwa ikikemea na itaendelea kukemea vitendo vya ubakaji, ulawiti na mapenzi ya jinsia moja pamoja na kuwachukulia hatua watakaojihusisha na vitendo hivyo kwani sheria zipo, huku akisisitiza kuwa, vitendo hivyo ni kinyume cha sheria na havitakiwi kifumbiwa macho.

“Niwaombe wazazi na jamii kila mmoja awe mlinzi wa kwanza kwa mtoto wake, kwani wanaowafuga waharifu hao ni sisi wenyewe wazazi.Unakuta mtu ameenda kuripoti kufanyiwa au mtoto wake kufanyiwa kitu fulani, lakini akiambiwa twende ukatuoneshe muhusika hatoi ushirikiano,”amesema Kihongosi na kuongeza;

“Lakini pia wapo baadhi ya wazazi ndiyo wamekuwa wakifuga vitendo hivi, kwani unakuta mtu anaambiwa mtoto wake mwizi akikamatwa anaenda kusema kuwa mtoto wake hawajai kuwa mwizi, kwaio nyinyi wenyewe ndiyo mnaokwamisha juhudi za Serikali katika kupingana na vitendo hivi,”.

Kihongosi yupo mkoani Arusha kwa ziara ya siku tatu, leo ikiwa ni siku yake ya pili akiwa wilayani Arumeru alikagua miradi ya maendeleo, kutembelea mashina ya CCM na mwisho alimaliza kwa kufanya mkutano wa hadhara eneo la Ngaramtoni, ambapo alisikiliza na kutatua kero za wananchi.