June 3, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Itunda-michezo ni uchumi ataka amani Tulia Cup

Na Mwandishi Wetu, Mbeya.

MKUU wa Wilaya ya Mbeya, Solomon Itunda, amewataka wachezaji wanaoshiriki mashindano ya Tulia Trust Uyole Cup 2026 kucheza kwa amani na utulivu, akisisitiza kuwa michezo ni afya, chanzo cha uchumi na nyenzo muhimu ya kujenga mshikamano katika jamii.

Itunda alitoa kauli hiyo wakati akifungua rasmi mashindano hayo yaliyofanyika katika Uwanja wa Mwawinji, ambapo mchezo wa Ngao ya Hisani kati ya Itezi United na Chipukizi FC ulitangulia kuashiria mwanzo wa msimu mpya wa michuano hiyo inayowakutanisha vijana kutoka maeneo mbalimbali ya Mbeya.

Alisema michezo inapaswa kutumika kama jukwaa la kuimarisha mahusiano mema miongoni mwa vijana, kujenga nidhamu na kuhamasisha ushirikiano badala ya kuzalisha migogoro na vurugu zinazoweza kuathiri maendeleo ya sekta hiyo.

Aidha, alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuwekeza katika sekta ya michezo kupitia ujenzi wa viwanja vya kisasa pamoja na sera na mipango inayowawezesha vijana kutumia michezo kama njia ya kujikwamua kiuchumi.

“Tumeendelea kuona timu zetu zikifanya vizuri, lakini hatua ya Dk. Tulia kuanzisha ligi hii imewafanya vijana kuwa bize na michezo, jambo ambalo ni jema kwa maendeleo yao,” alisema Itunda.

Kwa upande wake, Mratibu wa Michezo wa Taasisi ya Tulia Trust, Lugano Mwangosi, alisema taasisi hiyo imeendelea kudhamini mashindano hayo kwa lengo la kuibua vipaji, kukuza ajira na kuongeza fursa za kiuchumi kwa wananchi kupitia shughuli mbalimbali za michezo.

Mwangosi alisema mchezo wa Ngao ya Hisani uliowakutanisha mabingwa wa msimu uliopita, Itezi United na Chipukizi FC, ulimalizika kwa Itezi United kutwaa ushindi na kujinyakulia zawadi ya shilingi milioni 10 huku Chipukizi FC ikiondoka na shilingi milioni 5.

Aliongeza kuwa msimu huu wa Tulia Trust Uyole Cup umeboreshwa zaidi kwa kuongeza zawadi na vipengele vipya vya ushindani, ambapo bingwa atapata sh. milioni 10, mshindi wa pili milioni 5 na mshindi wa tatu milioni 3, sanjali na tuzo za mchezaji bora na kikundi bora cha hamasa.