Na Penina Malundo,Timesmajira
Mkuu wa Chuo cha Mafunzo ya Ulinzi wa Amani Tanzania (TPTC), Brigedia Jenerali George Itang’are amesema kozi maalum ya wanawake katika masuala ya ulinzi na usalama imezinduliwa rasmi kwa awamu ya pili ikilenga kuongeza ushiriki wao kikamilifu katika oparesheni za kulinda amani na utatuzi wa migogoro kwa matokeo chanya.
Brigedia Jenerali Itang’are ameyasema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati akifungua mafunzo hayo yanayofanyika katika Kampasi ya TPTC iliyopo Kunduchi, kwa ufadhili wa Serikali ya Japan kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo (UNDP) pamoja na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Wanawake (UN Women).
Amesema mafunzo hayo yanawahusisha wanawake 30 huku wanaume wachache wakijumuishwa ili kuongeza ufanisi wa mafunzo hayo na kujenga ushirikiano wa pamoja katika masuala ya ulinzi na usalama.

Kwa mujibu wake, amesema mafunzo hayo ni sehemu ya juhudi za serikali na taasisi za ulinzi na usalama kuhakikisha wanawake wanapata nafasi kubwa zaidi katika shughuli za kulinda amani ndani na nje ya nchi.
“Lengo si kuongeza idadi ya wanawake pekee, bali kuhakikisha wanashiriki kikamilifu katika shughuli za amani na usalama. Tunahitaji ushiriki wenye matokeo, si takwimu tu,” amesema Brigedia Jenerali Itang’are.
Aidha, amesema mbali na kozi hiyo, kuna programu nyingine zinazolenga kuwaandaa wanawake kushika nafasi za uongozi pamoja na mafunzo yanayohusu masuala ya kijinsia ndani ya vyombo vya ulinzi na usalama.

Brigedia Jenerali Itang’are amesema mafunzo hayo yanawakutanisha maofisa kutoka taasisi mbalimbali ikiwemo JWTZ, Jeshi la Polisi, Idara ya Uhamiaji na Jeshi la Magereza, hatua inayolenga kuimarisha ushirikiano katika operesheni za kulinda amani.
“Ulinzi wa amani unahusisha taasisi nyingi. Tunapokutana katika mafunzo kama haya tunajenga mahusiano mazuri ya kikazi na kuongeza uelewa wa pamoja kuhusu namna ya kutekeleza majukumu yetu katika misheni za amani,” amesema.

Kwa upande wake, Mwakilishi Mkazi wa UN Women nchini, Katherine Gufford amesema mafunzo hayo ni uwekezaji muhimu katika kukuza uongozi, ubora wa utendaji kazi na mustakabali wa taasisi za amani na usalama nchini.
Amesema Umoja wa Mataifa kupitia UN Women utaendelea kuunga mkono ajenda ya wanawake, amani na usalama kwa kutoa msaada wa kisera, kuimarisha uwezo wa taasisi, kufanya tafiti pamoja na kujenga ushirikiano na serikali na vyombo vya usalama

Naye Msaidizi Mkuu wa Kitengo cha Utawala wa UNDP, Fridah Mwakasyoka amesema mafunzo hayo ya mwaka huu ni awamu ya pili baada ya mafanikio ya awamu ya kwanza iliyofanyika mwaka jana.
“Mwaka jana tulifanya kazi kama hii kwa kushirikiana na TPTC na tulifanya vizuri, hali iliyotuwezesha kupata fedha za ziada kuendeleza mafunzo haya mwaka huu. Pia tumefanya maboresho katika mtaala ili kuendana na uhalisia wa masuala ya ulinzi na usalama,” amesema.

Ameongeza kuwa moja ya maboresho yaliyofanyika ni kufanya mafunzo hayo kuwa jumuishi zaidi kwa kuwashirikisha wanaume wachache tofauti na mwaka jana ambapo walikuwa wanawake watupu.

More Stories
Takukuru yageukia utapeli kwenye makundi ya WhatsApp
KCMC yaanza ujenzi kitengo maalumu cha moyo
Wanawake wahimizwa kugombea nafasi mbalimbali