Na Judith Ferdinand, Timesmajira Online- Mwanza
WITO umetolewa kwa wanawake kuachana na mtazamo hasi na woga,badala yake kujitokeza kugombea nafasi mbalimbali za uongozi katika taasisi tofauti nchini hapa.
Hayo yamebainishwa jana na Rais wa Serikali ya Wanafunzi wa Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA),kampasi ya Mwanza, Bertha Mollel wakati wa mahojiano na Majira ofisini kwake jijini Mwanza.
Mollel amesema,uongozi si suala la jinsia bali ni uwezo wa mtu kusaidia wengine, kusimamia changamoto na kuleta maendeleo kwa jamii inayomzunguka,hivyo wanawake wanapaswa kuwa na uthubutu wa kugombea nafasi mbalimbali za uongozi na kuachana na hofu.
Huku amesisitiza kuwa jamii nyingi bado haziwaamini wanawake katika nafasi za uongozi, jambo ambalo limekuwa likiwakatisha tamaa baadhi yao kushiriki katika maamuzi ya maendeleo ya jamii.
Amesema TIA kampasi ya Mwanza imeendelea kuwa sehemu muhimu ya kuwaunga mkono wanawake kuanzia utoaji wa elimu katika nafasi za elimu na ya kujitokeza kugombea nafasi mbalimbali za uongozi.
Pia Mollel, amesema Serikali ya wanafunzi imefanikiwa kutekeleza miradi mbalimbali yenye manufaa kwa wanafunzi wa chuo hicho ikiwemo ujenzi wa vimbweta vitano kwa ajili ya kujisomea katika mazingira bora zaidi.
Vile vile amesema kwa upande wa maendeleo ya teknolojia,taasisi hiyo imekuwa ikiendesha semina mbalimbali kuhusu masoko ya mtandao kwa wanafunzi wa chuo hicho ili kuwajengea uwezo wa kutumia mitandao ya kijamii na teknolojia kujitengenezea fursa za kiuchumi.
“Dunia ya sasa inaenda kidigitali, hivyo vijana wanapaswa kutumia vizuri mitandao ya kijamii kwa maendeleo yao badala ya matumizi yasiyo na tija,”amesema Mollel.
Hata hivyo amesema Serikali ya wanafunzi imeendelea kutoa elimu mbalimbali kwa wanafunzi ikiwemo elimu ya ulipaji kodi pamoja na kushirikiana na kampuni ya YAS katika kufanikisha michezo ya ‘interclass’ chuoni hapo.
Vilevile amesema changamoto ya ajira bado ni kubwa kwa vijana nchini hapa. Hivyo vijana wanapaswa kuamini katika ubunifu, kujituma na kutokata tamaa wanapokutana na changamoto mbalimbali za maisha.

More Stories
Takukuru yageukia utapeli kwenye makundi ya WhatsApp
TPTC yazindua awamu ya pili,Kozi ya wanawake masuala ya Ulinzi na Usalama
KCMC yaanza ujenzi kitengo maalumu cha moyo