
Na Moses Ng’wat, Tunduma.
MKUU wa Mkoa wa Songwe, Jabiri Omari Makame, amekabidhi hundi yenye thamani ya Sh. bilioni 1.4 kwa vikundi 59 vya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu vikiwa na wanufaika 289 kupitia mikopo ya asilimia 10, huku vijana wakitakiwa kutumia fursa hizo kwa bidii na kuachana na tabia ya kuchagua kazi.
Mikopo hiyo ilikabidhiwa Mei 21, 2026, ikienda sanjari na
ufunguzi wa Jukwaa la “Vijana na Wanawake Fursa Forum” lililofanyika Ukumbi wa Highclass Tunduma na kuhudhuriwa na washiriki zaidi ya 1000.

Akizungumza katika ufunguzi wa jukwaa hilo, Makame alisema mikopo hiyo inapaswa kutumika kwa uwajibikaji mkubwa ili kusaidia kuanzisha na kukuza miradi inayozalisha mapato pamoja na ajira kwa wananchi.
Aidha, katika jukwaa hilo, Makame alisema matumizi sahihi ya mikopo hiyo yatachangia kufanikisha malengo ya Dira ya Taifa 2050 inayolenga kukuza uchumi wa nchi na kuboresha maisha ya wananchi kwa ujumla.
Kwa mujibu wa Mkuu huyo wa Mkoa, hadi kufikia robo ya tatu ya mwaka wa fedha 2025/2026, Halmashauri ya Mji Tunduma tayari imetoa mikopo yenye thamani ya Shilingi bilioni 4.1 kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.

Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Mkoa wa Songwe, Dk. Frank Hawassi, aliwataka vijana na wanawake kutumia kila nafasi inayojitokeza badala ya kusubiri ajira rasmi au mtaji mkubwa kabla ya kuanza kujishughulisha.
Dk. Haule alisema vijana wengi waliofanikiwa leo walianza na shughuli ndogo zilizowajengea uzoefu, mtaji na kujiamini zaidi katika safari yao ya kiuchumi, huku akisisitiza kuwa kila kazi halali inaweza kuwa mwanzo wa mafanikio makubwa.


More Stories
Airtel, ZECO zaingia ushirikiano kuimarisha Huduma za Kidigitali
MSD kujenga ghala la kisasa lenye mita za mraba 3,900
Itunda-michezo ni uchumi ataka amani Tulia Cup