May 21, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali yaendelea kuboresha Sekta ya Elimu nchini

Na Zena Mohamed,TimesmajiraOline,Dodoma

SERIKALI  imeendelea kufanya maboresho mbalimbali katika sekta ya elimu ikiwemo sera, mitaala, idadi na ubora wa walimu, miundombinu pamoja na vitendea kazi kwa lengo la kuongeza ubora wa elimu nchini.

Hayo yamesemwa jijini hapa leo Mei 21,2026 na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda kwenye kikao cha kuwasilisha kwa wadau taarifa ya awali ya Kamati ya Mapitio ya Sheria ya Elimu Sura ya 353 ambapo amesema tayari sera mpya ya elimu imezinduliwa huku hatua inayofuata ikiwa ni kufanya maboresho ya sheria ili kuendana na mwelekeo huo mpya wa elimu.

Prof.Mkenda amesema serikali inaendelea kukusanya maoni kutoka kwa wadau mbalimbali ili kusaidia kuamua kama kutakuwa na sheria mpya ya elimu au maboresho zaidi ya sheria iliyopo.

“Tunakutana kwa ajili ya kupitia mapendekezo ya sheria ambayo tayari yamefanyiwa kazi. Sheria ya Elimu ya mwaka 1978 imefanyiwa marekebisho kadhaa, lakini sasa tunakusanya maoni yatakayosaidia kuamua kama tuje na sheria mpya au tufanye maboresho zaidi,” amesema Prof.Mkenda.

Amesema maoni yote yatakayokusanywa yatawasilishwa katika Baraza la Mawaziri kwa hatua zaidi za maamuzi huku serikali ikilenga kuhakikisha mchakato huo unakamilika ifikapo mwaka 2027.

Aidha, amewashukuru wadau wa sekta ya elimu kwa ushiriki wao katika kutoa maoni na mchango wao unaolenga kuboresha mfumo wa elimu nchini.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Caroline Nombo amesema wizara imejipanga kuyachakata na kuyafanyia kazi maoni yote yatakayowasilishwa na wadau.

Amesisitiza umuhimu wa washiriki kuwa wazi katika kutoa maoni yao ili kusaidia kupatikana kwa sheria bora na yenye manufaa kwa taifa.

Naye Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Wanu Hafidh Ameir amesema mchakato huo umechukua muda mrefu kwa lengo la kuhakikisha inapatikana sheria inayozingatia maoni ya wananchi wengi pamoja na wadau wa elimu.

Naye Mwakilishi wa Mwenyekiti wa Kamati ya Mapitio ya Sheria ya Elimu, Wakili Msomi Frida Mwela amesema kuwa baada ya vikao vya uhakiki, Kamati itaendelea kukamilisha hatua zinazohusu maandalizi ya rejea ya Kamati ambayo itasaidia katika uandaaji wa rasimu ya Sheria ya Elimu.

Ameongeza kuwa rasimu hiyo itazingatia masuala mahususi yatakayokuwa yamependekezwa na wadau kupitia mchakato wa mapitio ya Sheria hiyo.