Na Mwandishi wetu,Timesmajira
Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa kushirikiana na Sukos Kova Foundation wamezindua gari la kisasa la upasuaji linalotembea (mobile surgical operation unit) lenye thamani ya takribani shilingi bilioni 1.9, lengo likiwa ni kuimarisha upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Naibu Waziri wa Afya Dkt. Florence Samizi amesema uzinduzi huo ni sehemu ya mafanikio ya diplomasia ya afya chini ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, ambayo imeendelea kuimarisha ushirikiano wa kimataifa katika sekta ya afya.
Amesema “Gari hili lina uwezo wa kufanya upasuaji mdogo, uchunguzi wa kitabibu ikiwemo biopsy, pamoja na kutoa huduma za dharura kwa wagonjwa walioko maeneo ya mbali na vituo vya afya.”
“Litatumika pia katika huduma za mkoba (outreach) na kwenye majanga mbalimbali, likiwa na vifaa vya kisasa vinavyowezesha kutoa huduma za upasuaji moja kwa moja eneo la tukio, hivyo kupunguza gharama na muda wa kusubiri hospitalini.”ameongeza

Naibu Waziri huyo amesema gari hilo ni la kwanza la aina yake nchini na linatarajiwa kuboresha kwa kiasi kikubwa utoaji wa huduma za kibingwa, hususan kwa wagonjwa walioko pembezoni mwa nchi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dkt. Delilah Kimambo, amesema gari hilo litasaidia kuwafikia wananchi walioko maeneo ya mbali na kupunguza changamoto ya wagonjwa kushindwa kufika hospitali kubwa kwa wakati.
“Kuna wagonjwa wengi wanaohitaji upasuaji mdogo unaoweza kubadilisha maisha yao, lakini hawana uwezo wa kusafiri. Sasa huduma zitawafikia pale walipo.” Amesema

Aidha, amesema gari hilo pia litatumika katika majanga na dharura, likiwa na uwezo wa kutoa huduma za haraka na kuokoa maisha ya wananchi.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Sukos Kova Foundation, Rahma Kova, amesema ni heshima kubwa kwa taasisi yao kushiriki katika kufanikisha mradi huo wenye manufaa kwa wananchi, wakiwemo walioko vijijini.

“Wananchi hata walioko vijijini kwetu sisi ni heshima kubwa kuwa sehemu ya tukio hili muhimu na kuwa sehemu ya wafadhili wa programu hii muhimu.” Amesema
Ameongeza kuwa: “Tunaishukuru Serikali kwa ushirikiano mkubwa uliotuwezesha kupokea gari hili, na tuna imani kupitia Hospitali ya Taifa Muhimbili na Wizara ya Afya litatumika vizuri kuwafikia wananchi wengi zaidi.”
Rahma Kova alisema mradi huo ni mwanzo tu na taasisi yao itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali pamoja na Serikali ya China katika kuimarisha huduma za afya nchini.
“Huu ni mwanzo, tunatarajia kuendelea kusaidia zaidi serikali yetu katika kuboresha huduma kwa wananchi chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan.”amesema
Amehimiza wananchi kujitokeza kwa wingi pindi gari hilo linapofika kwenye maeneo yao ili kufaidika na huduma za kibingwa zinazotolewa karibu na jamii.

More Stories
Wateja wa Exim kupata huduma za kibenki kupitia Whatsap
Serikali yaendelea kuboresha Sekta ya Elimu nchini
Elimu unga uliorutubishwa yahitajika