May 20, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ripoti yaonya uharibifu Ziwa Victoria

*UNDP yatamani kuona wananchi wakinufaika na rasilimali za ziwa hilo

Na Judith Ferdinand, Timesmajira Online- Mwanza

JUMUIYA ya Afrika Mashariki imezindua ripoti ya mwaka 2025 kuhusu hali ya Bonde la Ziwa Victoria, ambayo ni ya kwanza ikiwa na sura tisa zinazoeleza kwa kina hali halisi ya ukanda wa ziwa hilo.

Ripoti hiyo imechambua changamoto mbalimbali zinazolikabili ziwa hilo, ikiwemo masuala ya ikolojia, mazingira, mipango miji, viwanda, ajira, utalii, pamoja na miundombinu ya barabara, reli na uchukuzi wa majini.

AkizungumzaMei 20,2026 katika mkutano kuelekea kilele cha maadhimisho ya Siku ya Ziwa Victoria yanayofanyika Mei 21, 2026, mkoani Mwanza,ikiwa ni miaka 30 tangu ajali ya kuzama kwa meli ya MV.Bukoba, Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Bonde la Ziwa Victoria,Jumuiya ya Afrika Mashariki,Dkt. Bwire Masinde,amesema hatua za haraka zinahitajika kuokoa ziwa hilo.

Ambapo amesema kwa mujibu wa ripoti hiyo imeonesha kuwa hali ya uvuvi haramu katika ukanda wa Ziwa Victoria inatisha.Kwani uvuvi wa kutumia sumu, nyavu haramu na teknolojia zisizoruhusiwa umeendelea kushamiri katika nchi za Tanzania, Kenya na Uganda, huku akizitaka mamlaka husika kuongeza doria na juhudi nyingine za kudhibiti uvuvi haramu ndani ya ziwa hilo.

“Tunaipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa hatua inazoendelea kuchukua, na pia Uganda imefanya juhudi kubwa. Hata hivyo, bado haitoshi. Wananchi wenyewe wanapaswa kuona jukumu la kupambana na uvuvi haramu kuwa ni lao kwani matumizi ya sumu katika uvuvi ni hatari kwa afya zao,”amesema Dkt. Masinde na kuongeza:

“Nadhani kuna kitu ambacho akipo sawa katika vichwa vyetu,inawezekanaje kula sumu kupitia samaki uliowavua mwenyewe,ukasambaza kwa ndugu zako na jirani zako.Ndio maana tunaendelea kushuhudia ongezeko la magonjwa kama saratani katika ukanda wa Ziwa Victoria. Miaka ya 1960 maradhi haya hayakuwa ya kawaida katika eneo hili. Lakini sasa hospitali kama Ocean Road nchini Tanzania, pamoja na hospitali za Kisumu nchini Kenya na Kampala nchini Uganda, zinapokea wagonjwa wengi wa saratani kutoka ukanda wa ziwa hili,”.

Amesema kuwa aina mbalimbali za samaki waliokuwa wakipatikana kwa wingi zimeanza kutoweka kutokana na uharibifu wa mazingira na uvuvi usio endelevu ikiwemo samaki aina ya sangara ambao ni muhimili kwa uchumi na chakula kwa wananchi wa ukanda huo kadhalika sato.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa UNDP Tanzania, Amon Manyama,amesema Ziwa Victoria ni rasilimali muhimu kwa maisha ya wananchi wa Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi,huku wakipenda kuona wananchi wote wakinufaika na rasilimali za ziwa hilo.

Amesema mchango wa UNDP ni kushiriki katika tafiti mbalimbali zinazolenga kubaini kiwango cha uchafuzi wa ziwa hilo na namna bora ya kukabiliana nao, ikiwemo matumizi ya teknolojia ya kuondoa magugu maji,ambayo inaweza kuyageuza kuwa mbolea na chakula cha mifugo, huku taka za plastiki zikirejelezwa na kutengenezwa bidhaa nyingine kupitia shughuli zitakazowanufaisha vijana na wanawake.

Amesema UNDP pia ina mchango katika juhudi za Serikali ambazo tayari imezifanya ikiwemo ya kupeleka “ambulence, kujenga vituo vya uangalizi wa hatari pamoja na kuimarisha huduma za doria kwa kutumia boti maalumu zinazosaidia wananchi wanaosafiri katika ziwa hilo.

Manyama amesema UNDP imefanya tathmini ya vivutio vya utalii katika mikoa ya Kanda ya Ziwa nchini Tanzania na kwamba kampeni ya kutangaza utalii huo itaanza hivi karibuni, ikianzia Kisiwa cha Ukerewe ambacho kimeonekana kuwa na vivutio vingi vya kipekee.

Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na Mazingira nchini Uganda, Dkt. Alfred Okidi, amesema juhudi za pamoja zinahitajika ili kuimarisha hali ya Ziwa Victoria, zikihusisha Serikali, wadau wa maendeleo, sekta binafsi na wananchi kwa ujumla.