May 20, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

CMCA yaendelea kuwa kichocheo cha ukuaji wa uchumi

Na Mwandishi Wetu,Timesmajira

OFISA Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMCA), Nicodemus Mkama amesema masoko ya mitaji yameendelea kuwa kichocheo muhimu cha ukuaji wa uchumi nchini huku akiahidi kuendelea kuweka mazingira bora kwa kampuni na sekta binafsi kushiriki kikamilifu katika uwekezaji.

Mkama ameyasema hayo jijini Dar es Salaam jana wakati wa hafla ya usajili wa hatifungani ya Kampuni ya EFTA katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), ambapo alisema kuwa mafanikio hayo yanaonyesha kuongezeka kwa imani ya wawekezaji katika masoko ya mitaji nchini.

Amesema mafanikio ya hatifungani ya EFTA yanaashiria hatua mpya katika jitihada za kuimarisha soko la mitaji pamoja na kukuza uwekezaji katika sekta ya uzalishaji nchini.

“Mafanikio haya yanaonyesha nguvu ya imani ya wawekezaji, uaminifu na dira ya pamoja ya kukuza uchumi wenye tija,” amesema Mkama.

Aidha, amesema EFTA imeweka historia kupitia mafanikio hayo baada ya kuvuka lengo la awali la ukusanyaji wa fedha.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya EFTA, Andrew Temu amesema mafanikio yaliyopatikana yanaakisi uaminifu mkubwa wa wananchi kwa taasisi hiyo pamoja na huduma zake.

Profesa Temu amesema fedha zilizopatikana kupitia hatifungani hiyo zitatumika katika ununuzi wa vifaa vya ujenzi na kuendeleza shughuli za uzalishaji, huku wakilenga zaidi kuwainua wakulima wadogo wadogo na wafanyabiashara ndogo ndogo.

“Hatifungani hii ni ya miaka mitano. Tunaishukuru Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kwa kutupa kibali na kujiridhisha na utendaji wetu wa kazi,” amesema Profesa Temu.

Amesema EFTA ililenga kukusanya Sh bilioni 15 lakini imefanikiwa kupata Sh bilioni 33.04, jambo linaloonyesha imani kubwa ya wawekezaji katika taasisi hiyo.

Awali, Mtendaji Mkuu wa EFTA, Nicomed Bohay amesema matokeo hayo yanaonesha wazi imani kubwa ya wawekezaji katika mkakati wa taasisi hiyo wa kuwekeza katika uchumi halisi.


Amesema EFTA itaendelea kuelekeza rasilimali hizo katika sekta zenye tija ili kuchochea ukuaji wa biashara, kuongeza ajira na kuharakisha maendeleo ya kiuchumi nchini.