Na Zena Mohamed,TimesmajiraOline,Dodoma
WAZIRI wa Ujenzi, Abdallah Ulega, amesema Serikali imejipanga kuendelea kuimarisha sekta ya ujenzi kupitia utekelezaji wa miradi ya kimkakati ya barabara na madaraja katika mwaka wa fedha 2026/27 ili kuharakisha maendeleo ya uchumi na usafirishaji nchini.
Ulega amesema hayo Bungeni Jijini hapa leo Mei 20,2026 wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Ujenzi ambapo alisema vipaumbele vya Wizara hiyo vinaendana na maono ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ambayo imeitambua sekta ya ujenzi kuwa mhimili muhimu wa kuwezesha usafirishaji fungamanishi na kuchochea mageuzi katika sekta mbalimbali za uzalishaji.

Amesema mafanikio ya utekelezaji wa Dira 2050, hususan katika ujenzi wa miundombinu, yatategemea ushirikiano kati ya Serikali na wadau mbalimbali wakiwemo wawekezaji binafsi kupitia mfumo wa Ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi (PPP).
Katika makadirio ya bajeti ya mwaka wa fedha 2026/27, Wizara ya Ujenzi imetengewa jumla ya Shilingi bilioni 97.1 kwa ajili ya matumizi ya kawaida. Kati ya fedha hizo, Shilingi bilioni 92.2 zimetengwa kwa mishahara huku Shilingi bilioni 4.8 zikielekezwa katika matumizi mengineyo.
Ameeleza kuwa bajeti ya maendeleo ya Wizara hiyo imefikia zaidi ya Shilingi trilioni 2.46 ambapo Shilingi trilioni 1.54 ni fedha za ndani na Shilingi bilioni 922.4 ni fedha za nje.
Ulega ameeleza kuwa kati ya fedha za ndani, zaidi ya Shilingi trilioni 1.04 zimetengwa kupitia Mfuko wa Barabara huku Shilingi bilioni 497.4 zikitoka Mfuko Mkuu wa Serikali kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.
Kwa mujibu wa Waziri huyo, fedha hizo zitaelekezwa katika utekelezaji wa miradi ya kimkakati ya barabara na madaraja inayolenga kuboresha usafiri, kuongeza ufanisi wa uchukuzi wa mizigo na huduma za kijamii pamoja na kuchochea shughuli za kiuchumi nchini.
Miongoni mwa miradi iliyotajwa kupewa kipaumbele katika mwaka wa fedha 2026/27 ni pamoja na barabara ya Soni – Bumbuli – Dindira – Korogwe ambayo ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuimarisha mtandao wa barabara nchini.


More Stories
Vipimo sahihi huwalinda wananchi,kupata bidhaa salama
Tanzania yasisitiza muhimu wa ushirikiano wa kikanda katika Nishati ya Nyuklia
Ripoti yaonya uharibifu Ziwa Victoria