May 20, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ulega:Bajeti 2026/27 itajenga msingi wa miundombinu ya kisasa

Na Zena Mohamed,TimesmajiraOline,Dodoma

WAZIRI  wa Ujenzi, Abdallah Ulega, akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa mwaka wa fedha 2026/27 bungeni leo Mei 20,2026 jijini  Dodoma, amesema bajeti hiyo imelenga kujenga msingi wa miundombinu ya kisasa, imara na inayokidhi mahitaji ya maendeleo ya Taifa kuelekea mwaka 2050.

Amesema mpango na bajeti ya Wizara umeandaliwa kwa kuzingatia mipango mikuu ya maendeleo ya Taifa ikiwemo Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (FYDP IV) pamoja na Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi 2025.

Ulega amelieleza bunge kuwa  bajeti ya mwaka 2026/27 ni ya kipekee kwa kuwa ndiyo bajeti ya kwanza katika utekelezaji wa maono yaliyopo kwenye Dira 2050 pamoja na Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2025. Alieleza kuwa Serikali imejikita katika kuimarisha miundombinu ya barabara na madaraja ili kukabiliana na ongezeko la mahitaji ya usafiri na changamoto za mabadiliko ya tabianchi.

Kwa mujibu wa Waziri huyo, sekta ya ujenzi imepewa nafasi kubwa katika kufanikisha mageuzi ya kiuchumi kupitia dhana ya “Usafirishaji Fungamanishi”, ambayo imetajwa kuwa moja ya vichocheo muhimu vya kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha biashara kikanda.

Aidha, miradi iliyopangwa kutekelezwa katika mwaka wa fedha 2026/27 inalenga kupunguza msongamano wa magari mijini, kuongeza ufanisi wa barabara zinazounganisha bandari na maeneo ya uzalishaji, pamoja na kusaidia ukuaji wa sekta za viwanda, kilimo, utalii na biashara.

Serikali pia imeweka mkazo katika ujenzi wa miundombinu inayostahimili athari za mabadiliko ya tabianchi pamoja na matumizi ya teknolojia za kisasa ili kuongeza ubora na ufanisi wa huduma za ujenzi nchini.

Katika hatua nyingine, Ulega amesema utekelezaji wa miradi hiyo utazingatia ushirikishwaji wa sekta binafsi kupitia mfumo wa Ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi (PPP), hatua inayolenga kuongeza uwekezaji na kasi ya utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo.

Kwa upande wa Chama Cha Mapinduzi, Waziri huyo amesema Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2025 imeelekeza Serikali kuendelea kutekeleza miradi ya kimkakati yenye manufaa kwa wananchi, huku Wizara ya Ujenzi ikiahidi kuhakikisha maelekezo yote yanayohusu sekta hiyo yanatekelezwa kikamilifu ifikapo mwaka 2030.