May 21, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Nchi za EAC zaonesha dhamira ya dhati ya kuimarisha ushirikiano wa kikanda

Na Mwandishi Wetu,Timesmajira

NCHI za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) zimeonesha dhamira ya dhati ya kuimarisha ushirikiano wa kikanda kupitia mifumo thabiti ya uoanishaji wa viwango, vipimo na upimaji.

Hatua hiyo itasaidia kuongeza maendeleo ya viwanda, kumlinda mlaji, kuondoa vikwazo visivyo vya kikodi pamoja na kuongeza ushindani wa bidhaa na huduma ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na katika masoko ya kimataifa.

Hayo yamesemwa hivi karibuni na Mkurugenz wa Uandaaji Viwango wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS) David Ndibalema, wakati’ Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ilipoitisha kikao cha 28 jijini Arusha cha Kamati ya Viwango ndani ya jumuiya hiyo kwa lengo la kuendelea kuimarisha uratibu wa masuala ya viwango, vipimo na upimaji katika nchi wanachama.

Ndibalema amesema Kamati hiyo ina jukumu la kuratibu na kufuatilia shughuli zilizo chini ya Sheria ya Kuanzisha Viwango, Vipimo bora na Upimaji ya mwaka 2006, huku ikilenga kuwezesha biashara, kurahisisha usafirishaji wa bidhaa na huduma pamoja na kuchochea maendeleo ya viwanda ndani ya ukanda wa Afrika Mashariki.

Amesema mkutano huo uliwakutanisha wajumbe kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, kamati ndogo za kitaalamu pamoja na washirika wa maendeleo, ikiwemo taasisi za kifedha, maendeleo na mashirika ya kimataifa yanayojihusisha na masuala ya viwango.

Aidha, amesema mkutano huo ulipitia maendeleo ya utekelezaji wa programu mbalimbali katika maeneo ya uanzishaji wa viwango, uhakiki wa ubora pamoja na kutathmini mafanikio yaliyofikiwa hadi sasa.

“Wajumbe walijadili na kuweka mpango wa utekelezaji wa mwaka 2026/27 ili kuendelea kuimarisha mifumo ya viwango, vipimo na upimaji katika ukanda huo,”alisema Ndibalema.

Amesema Sekretarieti iliitisha kikao cha kamati ya viwango ya jumuiya hiyo, kujadili mkakati wa kikanda wa kulinganisha mifumo ya ubora, ili kutatua changamoto ya mizigo inayopimwa kwenye mipaka ndani ya nchi moja, ikubalike nchi nyingine bila mfanyabiashara kulazimishwa kurudia kupima tena.

Kamati hiyo ya viwango ilipitisha viwango vipya takribani 90, ambavyo vitapelekwa ngazi ya juu kwa ajili ya kutangazwa kwenye Gazeti la Jumuiya ya Afrika ya Mashariki.

Kwa mujibu wa Ndibalema, idadi ya viwango ambavyo tayari vimeshalinganishwa kwenye Jumuiya ya Afrika ya Mashariki, ni takribani 2,163.

Amesema majadiliano hayo, yalilengai kuwezesha biashara, kupunguza vikwazo visivyo vya kikodi, na kurahisisha usafirishaji wa huduma na bidhaa ndani ya Jumuiya ya Afrika ya Mashariki.

Mkutano huo wa kamati ya viwango ulikutanisha nchi wanachama, kamati ndogo za kitaalam, washirika wa maendeleo, taasisi za kitaifa na kimataifa zinazojihusisha na uandaaji na ulinganishaji wa viwango.

“Lengo kuu la mkutano huu, ulikuwa kupitia maendeleo yaliyofikiwa katika utekelezaji wa program mbalimbali na kuweka mipango kwa ajili ya mwaka ujao wa fedha 2026/2027. Nia ni kusaidia maendeleo ya viwanda, kulinda afya ya mlaji, kuongeza ushindani wa bidhaa, na huduma ndani ya Jumuiya ya Afrika ya Mashariki, lakini pia kukuza biashara endelevu,”amefafanua zaidi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Viwango la Kenya (KEBS), Esther Ngari, alieleza kuwa kamati ndogo zilizokutana zilijadili kwa kina uoanishaji wa viwango katika Jumuiya ya Afrika Mashariki.

“Tunataka tuwe tunafanya upimaji unaolingana katika maabara zetu. Hivi viwango vitatusaidia kufanya biashara kati ya nchi na nchi, mara tu tunapooanisha viwango hivyo. Tulipitia na kujadili ripoti za mwaka na mipango kazi ya kamati ndogo za mwaka 2026/2027,”amesema Ngari.

Ametaja kamati zilizowasilisha ripoti zao, ni kamati ndogo ya kiufundi ya EASC inayojadili kuhusu uhakiki wa ubora (QATSC), kamati ndogo ya kiufundi ya EASC inayoangalia vipimo na mizani (EAMET) na Jukwaa la Codex la EAC.

Nyingine ni kamati ndogo ya kiufundi ya EASC inayojadili upimaji (TTSC), Jukwaa la EASC linaloangalia vikwazo vya kiufundi katika Biashara (TBT Forum); na kamati ndogo ya kiufundi ya EASC inayopitia ulinganishaji wa viwango (SMC).