Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online
KATIKA juhudi za kuhakikisha vijana wazawa wanapata fursa za ajira, mwekezaji wa ndani kupitia kituo cha mafuta cha kisasa cha CMT kilichopo eneo la Magorofani, Uyole jijini Mbeya, ameendelea kuweka mazingira yatakayowawezesha vijana kujishughulisha kiuchumi badala ya kukaa vijiweni bila shughuli.
Mkurugenzi mtendaji wa kituo cha mafuta cha CMT, Celtel Mahenge, amesema hayo wakati wa hafla ya uzinduzi wa kituo hicho, akieleza kuwa uwekezaji huo unalenga kuongeza ajira kwa vijana pamoja na kuchochea mzunguko wa fedha katika jamii.
Mahenge amesema wananchi wa Uyole na maeneo ya jirani watanufaika kwa kupata huduma bora za mafuta sambamba na ukuaji wa shughuli za kiuchumi zitakazotokana na uwekezaji huo.

“Uwekezaji huu utasaidia vijana wengi kupata shughuli za kufanya kwani ninatarajia kuajiri vijana 15…….ninaamini hatua hiyo itasaidia kupunguza tatizo la vijana kukaa mtaani bila kazi,” amesema Mahenge.
Amesema mbali na kutoa ajira, kituo hicho kitasaidia kuongeza mzunguko wa fedha na kuchochea maendeleo ya kiuchumi kwa wananchi wa eneo hilo kupitia biashara na huduma mbalimbali zinazohusiana na shughuli za kituo hicho.
Mgeni rasmi katika hafla hiyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzaga, amepongeza uwekezaji huo akisema miradi ya aina hiyo ina mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa maeneo ya mijini na kusaidia vijana kupata ajira.
“Uwekezaji huu ni mfano mzuri wa namna sekta binafsi inavyoweza kushirikiana na Serikali katika kuchochea maendeleo na kutoa fursa za ajira kwa vijana,” amesema Kuzaga.

Mkazi wa Uyole Kati, Juma Hassan, amesema uwepo wa kituo hicho utasaidia vijana wengi waliokuwa hawana ajira na baadhi yao kujihusisha na vitendo visivyofaa kama uzururaji na matumizi ya dawa za kulevya.
“Sisi tunamshukuru mwekezaji huyu kwa kutuona vijana. Hata kama watapata wachache, bado itasaidia kupunguza idadi ya vijana wanaokaa mtaani bila kazi,” amesema Juma.
Serikali imekuwa ikiendelea kuhamasisha uwekezaji wa ndani kama njia ya kuongeza ajira kwa vijana na kuchochea maendeleo ya uchumi katika maeneo mbalimbali nchini, huku sekta binafsi ikitajwa kuwa nguzo muhimu katika kupunguza changamoto ya ukosefu wa ajira.

More Stories
CRDB Foundation,Zuchu wazindua jukwaa la “Zuchu – IMBEJU Masterclass
Hatifungani ya kwanza yazinduliwa iTrust
Ofisi ya Msajili wa Hazina yafanya mazungumzo na Balozi wa China