Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online
DIWANI wa viti maalum Mbeya jiji, Atu Msai, ameonyesha mfano wa kuhamasisha jamii kujali afya kwa kushiriki mbio za Mbeya Betika Tulia Marathon na kufanikiwa kukimbia kilomita tano pamoja na kujinyakulia medali.
Msai alishiriki mbio hizo akiwa ameambatana na Spika mstaafu wa Bunge na Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU), Tulia Ackson, pamoja na baadhi ya madiwani wa Jiji la Mbeya katika mbio zilizofanyika mwishoni mwa wiki katika viwanja vya Sokoine.
Akizungumza baada ya kukamilisha mbio hizo, Msai amesema ushiriki wake unalenga kuhamasisha wananchi kujenga utamaduni wa kufanya mazoezi mara kwa mara ili kuboresha afya na kujikinga dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza.

Amesema wananchi wanapaswa kutumia michezo kama sehemu ya maisha yao ya kila siku kwa kuwa mazoezi yana mchango mkubwa katika kuimarisha afya ya mwili na akili.
Katika mashindano hayo, Msai alifanikiwa kukamilisha mbio za kilomita tano na kutunukiwa medali ikiwa ni ishara ya ushindi na kuthamini juhudi zake katika kushiriki mbio hizo za kijamii.
Mbio za Mbeya Betika Tulia Marathon zimeendelea kuwa jukwaa muhimu la kuhamasisha wananchi kushiriki michezo, kuimarisha mshikamano wa kijamii na kutoa fursa kwa wajasiriamali kufanya biashara na kujipatia kipato.
Mbeya Betika Tulia Marathon imekuwa miongoni mwa matukio makubwa ya michezo katika mkoa wa Mbeya, yakilenga kuhamasisha mazoezi ya mwili, kuunganisha jamii na kuongeza mwamko wa afya kwa wananchi kupitia ushiriki wa viongozi, wanamichezo na wananchi wa kawaida.

More Stories
CRDB Foundation,Zuchu wazindua jukwaa la “Zuchu – IMBEJU Masterclass
Hatifungani ya kwanza yazinduliwa iTrust
Ofisi ya Msajili wa Hazina yafanya mazungumzo na Balozi wa China