Na Zena Mohamed,TimesmajiraOline,Dodoma
WAZIRI wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Rhimo Nyansaho, amesema hali ya ulinzi na usalama katika mipaka ya Tanzania imeendelea kuwa shwari katika mwaka wa fedha 2025/26 licha ya kuwepo kwa changamoto mbalimbali za kiusalama katika baadhi ya maeneo ya mipakani.
Dkt. Nyansaho amesema hayo leo Mei 19, 2026 bungeni jijini Dodoma wakati akiwasilisha Bajeti ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kwa mwaka wa fedha 2026/27.
Amesema mipaka ya Tanzania yenye urefu wa kilomita 5,923.41 inayojumuisha mipaka ya nchi kavu, anga na maji imeendelea kulindwa kwa ufanisi na vyombo vya ulinzi na usalama.

Kwa mujibu wa Waziri huyo, hakuna tukio lolote lililoashiria uvunjifu wa amani kati ya Tanzania na nchi jirani zilizopakana nayo ambazo ni Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Kenya, Malawi, Msumbiji, Rwanda, Uganda na Zambia pamoja na mipaka ya Bahari ya Hindi inayohusisha Comoros na Shelisheli.
Hata hivyo,amesema baadhi ya changamoto zimeendelea kujitokeza ikiwemo uharibifu wa alama za mipaka, ukosefu wa barabara za ulinzi pamoja na migogoro ya ndani katika baadhi ya nchi jirani.
Akizungumzia mpaka wa Tanzania na Burundi wenye urefu wa kilomita 468.85, Dkt. Nyansaho alisema hali ya usalama ni shwari huku Wizara kupitia Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania ikiendelea kushirikiana na vyombo vingine vya usalama kuimarisha ulinzi katika eneo hilo.
Kwa upande wa mpaka wa Tanzania na DRC wenye urefu wa kilomita 554, Waziri huyo alisema changamoto kubwa inaendelea kusababishwa na mapigano yanayoendelea Mashariki mwa DRC kati ya Jeshi la nchi hiyo na makundi yenye silaha hususan kundi la M23.

Amesema kundi hilo limeendelea kushikilia maeneo mbalimbali ya kimkakati katika majimbo ya Kivu Kaskazini na Kusini ikiwemo miji ya Goma, Bukavu na Uvira jambo linaloongeza changamoto za kiusalama katika mpaka huo.
“Wizara kupitia JWTZ imeendelea kufuatilia hali hiyo kwa ukaribu ikiwemo kufanya doria mara kwa mara katika Mpaka huu,”amesema Dkt. Nyansaho.
Aidha, Waziri huyo amesema hali ya usalama katika mpaka wa Tanzania na Kenya wenye urefu wa kilomita 1,187 imeendelea kuwa shwari huku kazi ya kuimarisha alama za mpaka huo ikiendelea kufanywa kwa ushirikiano wa wataalam kutoka Tanzania na Kenya.
Kwa upande wa mpaka wa Tanzania na Malawi wenye urefu wa kilomita 394,amesema hali ya usalama imeendelea kuwa tulivu bila kuwepo matukio yenye viashiria vya kuhatarisha usalama wa Taifa.

More Stories
Njombe yaibuka kitovu cha madini adimu
CRDB Foundation,Zuchu wazindua jukwaa la “Zuchu – IMBEJU Masterclass
iTrust yazindua Hatifungani ya kihistoria nchini