May 20, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dkt.Nyansaho aeleza vipaumbele maendeleo ya jeshi bajeti 2026/27

Na Zena Mohamed,TimesmajiraOline,Dodoma

WAZIRI  wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Rhimo Nyansaho, leo Mei 19, 2026 amewasilisha Bungeni Bajeti ya Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2026/27, akieleza mkakati wa Serikali wa kuendelea kuimarisha uwezo wa ulinzi, usalama na maendeleo ya taasisi za kijeshi nchini.

Katika hotuba yake, Waziri Nyansaho amesema Serikali itaendelea kuliimarisha Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania kwa kulipatia zana na vifaa vya kisasa vya kijeshi, mifumo ya mawasiliano ya kiteknolojia pamoja na kuendeleza rasilimali watu ili kuongeza ufanisi wa utekelezaji wa majukumu ya ulinzi wa Taifa.

Miongoni mwa maeneo ya kipaumbele yaliyotajwa katika mwaka wa fedha 2026/27 ni pamoja na kuboresha mazingira ya kazi kwa wanajeshi kupitia huduma bora za afya, makazi, mafunzo, mazoezi pamoja na matunzo ya vifaa na zana za kijeshi.

Aidha,amesema  Serikali imeeleza dhamira ya kuendelea kuimarisha Jeshi la Kujenga Taifa kwa kuboresha miundombinu yake ili liweze kupokea vijana wengi zaidi watakaopata mafunzo ya awali ya kijeshi sambamba na stadi mbalimbali za kazi kwa ajili ya maendeleo ya Taifa.

Katika hatua nyingine, Wizara hiyo imeweka mkazo katika kuimarisha Jeshi la Akiba pamoja na kuendeleza na kulinda miradi ya kimkakati yenye maslahi mapana kwa Taifa.

Hotuba hiyo pia imebainisha mpango wa kuimarisha mashirika na taasisi za utafiti wa masuala ya kijeshi pamoja na kuanzisha viwanda vipya vya ulinzi vitakavyozalisha bidhaa kwa matumizi ya kijeshi na kiraia. Serikali pia imeeleza kuwa itaendelea kushirikiana na sekta binafsi katika kuanzisha viwanda hivyo ili kuongeza uzalishaji na ajira nchini.

Katika eneo la ushirikiano wa kimataifa, Waziri Nyansaho amesema Tanzania itaendelea kuimarisha ushirikiano wake na Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afrika, Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika pamoja na Jumuiya ya Afrika Mashariki katika masuala ya ulinzi na usalama wa kikanda.

Pia, Wizara hiyo imeahidi kuendelea kushirikiana na mamlaka za kiraia katika kukabiliana na majanga na dharura mbalimbali pale inapohitajika, ikiwa ni sehemu ya mchango wa Jeshi kwa jamii na Taifa kwa ujumla.