Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online
BARAZA Kuu la Waislam Tanzania (BAKWATA) limetangaza kuwa sikukuu ya Idd El-Adha mwaka huu itaadhimishwa Mei 27, kwa mujibu wa kalenda ya Kiislamu.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa BAKWATA, Nuhu Jabiri Mruma amesema swala ya kitaifa ya Idd El-Adha itafanyika Mkoa wa Dar es Salaam katika Msikiti wa Mfalme Mohamed wa Nne, uliopo Makao Makuu ya BAKWATA, wilayani Kinondoni.
Amesema swala hiyo itaanza saa 1:30 asubuhi na baadaye kuendelea na baraza la Idd litakalowakutanisha viongozi wa dini, waumini pamoja na wageni mbalimbali kwa ajili ya nasaha na mawaidha ya kidini.

Kwa niaba ya Mufti wa Tanzania, Abubakari Bin Zubeir Bin Ally, Mruma amewatakia waislam wote nchini maandalizi mema ya sikukuu hiyo huku akiwataka kuitumia siku hiyo kuimarisha mshikamano, upendo na kusaidiana katika jamii.
Amesema BAKWATA imekamilisha maandalizi ya maadhimisho hayo na kuwasihi waumini kujitokeza kwa wingi kushiriki ibada pamoja na shughuli mbalimbali za kijamii zitakazoambatana na sikukuu hiyo.
Idd El-Adha ni moja ya sikukuu kubwa kwa waislam duniani, huadhimishwa baada ya kukamilika kwa ibada ya Hijja katika mji mtakatifu wa Makka, Mecca. Sikukuu hiyo hujulikana pia kama “Sikukuu ya Kuchinja” kutokana na ibada ya kuchinja wanyama inayofanywa na waislam wenye uwezo kama ishara ya utiifu kwa Mwenyezi Mungu.
Sherehe hizo huambatana na swala maalum ya Idd, kutembeleana, kusaidia wahitaji pamoja na kugawana nyama kwa ndugu, majirani na watu wenye uhitaji. Nchini Tanzania, maadhimisho ya Idd El-Adha kwa miaka mingi yamekuwa yakiratibiwa na BAKWATA katika ngazi ya taifa na mikoa mbalimbali.

More Stories
Vyuo vitano kunufaika na mradi wa UTT
Kamati ya Bunge yakoshwa na utendaji wa TMDA
Airtel Afrika Foundation yaunganisha Shule 3,296 na Intaneti