Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online- Tabora
HALMASHAURI ya Manispaa ya Tabora imetoa motisha kwa walimu na shule za sekondari zilizofanya vizuri zaidi katika masomo mbalimbali kwenye mitihani ya taifa ya kidato cha nne,sita pamoja na kujipima wa kidato cha 2 kwa mwaka 2025.
Akitoa taarifa kwenye kikao cha Baraza la Madiwani, Mkurugenzi wa halmashauri hiyo Dkt.John Pima, ameeleza kuwa wametoa motisha hiyo kuwatia moyo walimu pamoja na shule zao ili waendelee kufanya vizuri zaidi.
Amefafanua kuwa kwa mwaka wa masomo 2025 halmashauri hiyo ilishika nafasi ya kwanza kimkoa kati ya halmashauri 8 katika mitihani ya taifa ya kidato cha sita, nne na upimaji wa kidato cha pili.
Dkt Pima amesema,kwa ujumla shule zote katika manispaa hiyo zilifanya vizuri katika mitihani hiyo ikilinganishwa na mwaka uliopita sababu kuu ikitajwa kuwa ni juhudi na weledi wa walimu katika kufundisha watoto hao.
Ambapo katika mitihani ya kidato cha nne,walimu wa shule za sekondari za kata ambao masomo yao yalipata ufaulu mkubwa zaidi wamezawadiwa cheti na fedha taslimu sh.100,000.
Walimu hao ni Agnes Ndele wa shule ya sekondari Nkumba (Kiswahili), David Mwalwisi wa shule ya sekondari Nyamwezi (Hisabati), Veronika Maziku shule ya sekondari Fundikira (Biolojia) na Msafiri Mkinde wa sekondari ya Nyamwezi (Kemia).
Wengine ni Boaz Ewiso (Uraia), Ruben Lishinu (Jiografia), Boniphace Wambura (Fizikia) wote kutoka sekondari ya Nkumba huku Paulo Kamlali wa sekondari ya Nyamwezi (Historia) na Damian Ndibalema wa sekondari ya Misha (Kiingereza).
Ametaja shule zenye idadi kubwa ya watoto zilizofanya vizuri katika mitihani hiyo na kuzawadiwa cheti na kiasi cha sh.300,000 ni sekondari ya Milambo, Ipuli na Kazima.
Hata hivyo amesema shule tatu zilizoshika nafasi ya kwanza hadi tatu kwa matokeo ya jumla na kuzawadiwa cheti na fedha taslimu kuwa ni shule ya sekondari ya wavulana Tabora,shule ya sekondari ya wasichana Tabora na sekondari Itaga.
Shule nyingine zilizofanya vizuri na kuzawadiwa cheti na fedha taslimu ni sekondari ya Nkumba,Itonjanda na Nyamwezi.
Mstahiki Meya wa Halmashauri hiyo Ghulam Remtullah amesema, zawadi hizo zitaongeza ushindani katika shule zote huku akisisitiza kuwa wataendelea na utaratibu huo ili kuinua zaidi kiwango cha ufaulu kwa shule zote za sekondari na msingi katika halmshauri hiyo.

More Stories
Serikali ya Samia yaleta mageuzi ya elimu Tarime vijijini
Kapinga: Serikali yaboresha Elimu, Afya, Kilimo Mbinga
Mwaselela: Rais Samia aimarisha ukaribu na wananchi