May 15, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Madaktari Mloganzila wanufaika na mafunzo maalum ya tiba za mifupa

Na Mwandishi wetu,Timesmajira

Hospitali ya Taifa Muhimbili- Mloganzila imeendelea kuimarisha huduma za mifupa na ajali kupitia kambi maalum ya mafunzo ya siku tatu iliyolenga kuboresha mbinu za matibabu ya ulemavu wa mifupa na majeraha ya ajali, ikiwa ni sehemu ya mpango wa kuongeza ubora wa huduma za kibingwa nchini.

Akizungumza kuhusu kambi hiyo, Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za upasuaji Dkt. Godlove Mfuko amesema mafunzo hayo yaliyofanyika kuanzia Jumatano hadi Ijumaa yamelenga kuwawezesha wataalamu kutoa huduma za kisasa na za kina kwa wagonjwa wenye changamoto mbalimbali za mifupa.

Dkt. Mfuko amesema dira ya hospitali ni kuhakikisha Mloganzila inakuwa kituo kikuu cha huduma za mifupa na ajali kinachoweza kushughulikia matatizo yote ikiwemo nyonga, magoti, majeraha ya ajali na ulemavu wa aina mbalimbali kwa mfumo mmoja wa matibabu.

Ameongeza kuwa programu za upasuaji wa nyonga na magoti ambazo zinaendelea kutekelezwa tayari zimefikia takribani wagonjwa 400, hatua inayoonesha maendeleo makubwa katika utoaji wa huduma hizo.

Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Upasuaji wa Mifupa na Ajali, MNH – Mlonganzila Dkt. Magdalena Mbeyale amesema mafunzo hayo yamewapa washiriki uelewa mpana kuhusu matumizi ya teknolojia na mbinu mpya za kurekebisha ulemavu wa mifupa.

Naye Mkufunzi wa mafunzo hayo ambaye ni Daktari Bingwa Mbobezi Mshauri wa Mifupa na Ajali kutoka Hospitali ya Manchester Royal Infirmary, Dkt. Amer Shoaib amesema pamoja na kutoa elimu ya kitaalamu, wamekabidhi msaada wa baadhi ya vitaa vya upasuaji wa mifupa vitakavyosaidia kuboresha huduma kwa wagonjwa.