Na Mwandishi wetu,Timesmajira
Tanzania huzalisha zaidi ya tani 14 milioni za taka kwa mwaka ambazo zinatajwa kuwa rasilimali inayoweza kuongeza kipato.
Hayo yameelezwa katika kikao cha wadau kilichoandaliwa na Baraza la Usimamizi wa Mazingira (NEMC).
Wadau katika kikao hicho wameelezwa kuwa asilimia 40 hadi 50 ya taka hizo huzalishwa katika miji mikubwa kama Dar es Salaam, Mwanza, Arusha, Dodoma, Mbeya na Tanga.
Akizungumza katika kikao hicho Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira Balozi Baraka Luvanda amesema;
“Kadri dunia inavyoelekea katika uchumi wa kijani na maendeleo endelevu, usimamizi wa taka na urejelezaji si tu suala la mazingira bali pia ni fursa ya kiuchumi”
Amesema ni wajibu wa serikali na wadau kuhakikisha tunajenga mfumo jumuishi, unaotambua mchango wa kila mdau na unaowezesha ukuaji wa sekta hii kwa tija zaidi.

Katika kikao hicho ambacho kilijumuisha wadau waokota taka rejeshi wa mkoa wa Dar es Salaam ilielezwa kuwa waokota taka rejeshi bado wanakabiliwa na changamoto ya kipato kidogo licha ya mchango wao muhimu katika kupunguza wingi wa taka na kurahisisha urejelezi wa taka.
Balozi Luvanda amesema mchango wa waokota taka rejeshi na waokota chuma chakavu ni muhimu.
“Ninyi ni sehemu ya mfumo wa usimamizi wa taka ambao kwa muda mrefu umechangia kwa kiasi kikubwa kupunguza taka zinazopelekwa dampo, kuongeza viwango vya urejelezaji, kutoa ajira na kipato kwa maelfu ya wananchi, na kuchangia katika kupunguza uzalishaji wa taka” amesema

Mkurugenzi wa NEMC Dk Immaculate Sesemi amesema mazingira ni sehemu muhimu ya afya, akili na maendeleo ya kiuchumi ya taifa.
Dk Sesemi amesema NEMC imepewa jukumu la kusimamia usalama wa mazingira ya nchi nzima.
“Leo hii, wadau wa urejelezaji, wawekezaji wa teknolojia za mazingira, waokota taka na wabunifu wa suluhisho za kijani wana mchango mkubwa katika kupunguza uchafuzi wa mazingira, kuongeza ajira za kijani na kuchochea uchumi endelevu wa Taifa” amesema Dkt Sesemi
Wadau katika kikao hicho kadhalika walielezwa madhara ya ongezeko la taka kuwa ni pamoja na kuziba kwa mifereji ya maji,Mafuriko ya mara kwa mara,Kuongezeka kwa magonjwa ya mlipuko,Uchafuzi wa mazingira,Kuongezeka kwa gharama za usafishaji wa miji nakupotea kwa rasilimali ambazo zingeweza kurejelezwa na kuingizwa tena kwenye uchumi.

More Stories
TAKUKURU Kinondoni yaainisha mafanikio Januari_ Machi 2016
Serikali yafikisha Umeme Katika Migodi 289 ya Wachimbaji Wadogo
Vipaumbele tisa bajeti Maliasili na Utalii