Na Judith Ferdinand, Timesmajira Online -Mwanza
JESHI la Polisi mkoani Mwanza limetakiwa kujenga uhusiano mzuri na wananchi ili kuimarisha ulinzi na usalama katika jamii pamoja na kuchochea maendeleo mbalimbali ya mkoa na taifa.
Wito huo umetolewa Mei 9,2026 na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Said Mtanda,katika maadhimisho ya Siku ya Familia ya Polisi(Police Family Day), kimkoa yaliofanyika uwanja wa Nyamagana jijini hapa.ambapo amesisitiza ushirikiano kati ya polisi, wananchi na vyombo vingine vya usalama kuwa ni msingi wa amani na maendeleo.

Mtanda amesema,pamoja na jukumu la ulinzi na usalama kusimamiwa na jeshi hilo lakini wananchi ni wadau muhimu katika kuhakikisha amani inadumu nchini hapa,hivyo utaratibu wa kuadhimisha Siku ya Familia ya Polisi inawaleta pamoja na kuimarisha ushirikiano.
“Nawapongeza kuendelea kuimarisha usalama wa mkoa,bila usalama hatuwezi kuzungumzia maendeleo ya kijamii, kisiasa na kiuchumi.Mchango wa Mkoa wa Mwanza wa sh.trilioni 7.2,katika pato la taifa,ni kielelezo cha mazingira salama yanayowezesha wananchi kufanya shughuli za uzalishaji na maendeleo ya kiuchumi,”amesema Mtanda.
Sanjari na hayo,Mtanda amesema Serikali imeendelea kuboresha mazingira ya kazi kwa jeshi hilo kupitia upandishaji vyeo kwa maofisa na askari, kuongeza vitendea kazi pamoja na ujenzi wa vituo vya polisi.

Kwa upande wake,Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) Wilbrod Mutafungwa,amesema hali ya usalama mkoani humo ni shwari tangu kumalizika kwa uchaguzi mkuu mwaka 2025, huku wananchi wakiendelea na shughuli zao za uzalishaji kwa amani.
DCP.Mutafungwa amesema,licha ya kuwepo kwa baadhi ya matukio ya uhalifu jeshi hilo limekuwa likiyadhibiti kwa ushirikiano wa wananchi,ambapo watuhumiwa wamekuwa wakikamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.
“Jeshi la Polisi limeendelea kudhibiti matukio ya unyang’anyi, ujambazi pamoja na kuimarisha usalama barabarani kwa kushirikiana na wananchi,”amesema DCP.Mutafungwa.


More Stories
Maisha ya machozi yageuka matumaini
DCEA yakamata kemikali bashirifu lita 66,048
CHWs waimarishwa kuwabaini watoto wenye changamoto