
Na Moses Ng’wat, Ileje.
MKUU wa Mkoa wa Songwe, Jabiri Omari Makame, amewaagiza wafanyabiashara wa nafaka mkoani humo kuacha kutumia madebe na makopo katika kupima mazao, badala yake watumie mizani sahihi ili kuhakikisha uwazi na haki katika biashara hiyo.
Agizo hilo alilitoa Mei 6, 2026, wakati wa ziara yake wilayani Ileje, katika Kata ya Isongole, Kijiji cha Ilulu, alipokuwa akisikiliza na kutatua kero za wananchi pamoja na kukagua miradi ya maendeleo.
Alilazimika kutoa agizo hilo mara baada ya kufika katika kijiji cha Ikumbilo Wilayani humo na kujionea wafanyabiashara katika eneo hilo wakitumia vipimo vya madebe na makopo badala ya mizani inayokubalika kisheria
Makame amesema matumizi ya mizani yatasaidia kulinda maslahi ya wakulima na wanunuzi, kuondoa udanganyifu katika vipimo na kuimarisha mfumo rasmi wa biashara ya mazao ya nafaka mkoani humo.
Alisisitiza kuwa utaratibu wa kutumia vipimo visivyo rasmi umekuwa ukilalamikiwa kwa muda mrefu, huku baadhi ya wafanyabiashara wakidaiwa kuwanyonya wakulima kwa kutumia vipimo visivyo na uwiano sahihi.
Kutokana na hali hiyo, Mkuu huyo wa Mkoa aliwaelekeza viongozi na wataalam wa Halmashauri kusimamia kwa karibu utekelezaji wa agizo hilo ili kuhakikisha wafanyabiashara wote wanazingatia matumizi ya mizani.
Aliongeza kuwa hatua hiyo itachochea uaminifu katika soko la nafaka, kuongeza mapato kwa wakulima na wafanyabiashara, na kuchangia ukuaji wa uchumi wa mkoa.
Ziara hiyo ni sehemu ya kampeni ya “Serikali Nyumbani Kwako,” inayotekelezwa na ofisi ya mkuu wa mkoa kwa lengo la kusogeza huduma karibu na wananchi, kusikiliza changamoto zao na kuzitafutia ufumbuzi wa haraka.
Kupitia kampeni hiyo, Serikali inalenga pia kuharakisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kuboresha ustawi wa wananchi katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Songwe.

More Stories
Prof.Mbawara:TMA yakamilisha ufungaji wa mitambo miwili ya uangazi wa hali ya hewa
PBPA yapongezwa kwa usimamizi wa upatikanaji wa Mafuta nchini
Ujenzi wa Kituo cha Kupunguza Msukumo wa Mafuta Handeni wafikia asilimia 77