May 3, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Shule za Sekondari nane zanufaika na Kitulo Garden Maratho

Na Agnes Alcardo, Timesmajira Online. Makete

MKURUGENZI wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Ephraim Mafuru, ameupongeza uongozi wa Kampuni ya Event and Promotion, kwa kuandaa mbio za Kitulo Garden Marathon, ambazo zimesaidia katika kukuza utalii wa nchi pamoja na kurudisha kwa jamii.

Mafuru amesema ni vyema wadau mbalimbali wakaendelea kujitokeza na kufanya bunifu mbalimbali zenye tija, ili kuleta maendeleo kwa jamii na nchi kwa ujumla.

Akizungumza mapema leo kwenye mbio za Kitulo Garden Marathon, zilizofanyika Mei 2, 2026 katika Hifadhi ya Kitulo, iliyopo katika Wilaya ya Makete mkoani Njombe, Mafuru ambaye alihudhuria kama mgeni rasmi akimuwakilisha Waziri wa Maliasili na Utalii, Ashatu Kijaji, amesema, utalii kupitia michezo umeendelea kuwa injini mpya ya kuongeza mapato kwa jamii, husuani katika upande wa michezo ambayo mara nyingi hurudisha kwa jamii.

Amesea, mbali na utalii wa michezo uliofanyika, vilevile wananchi wengi wamejipatia kipato kwa kuuza bidhaa na kutoa huduma mbalimbali kama huduma ya malazi, vyakula, vinywaji, kazi za mikono na huduma za usafiri hali hii inaonyesha kwamba utalii ni jumuishi.

Aidha, Mafuru ameongeza kuwa, marathon hiyo pia imechangia kurudisha kwa jamii kwa kutoa kompyuta 40 katika shule nane za sekondari zinazopatikana katika wilaya ya Makete.

“Hali hii inachagiza vitu vinne muhimu ambavyo ni unakimbia, unatangaza, unahifadhi lakini pia unasaidia kwa jamii, hii itaongeza ushiriki wa jamii katika kuhifadhi maliasili”, amesema Mafuru.

Naye Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi TANAPA Godwell Meing’ataki, ambaye ni Mkuu wa Kanda ya Kusini amesema, tukio hilo limefungua fursa kwa wajasiriamali na kuwafanya wananchi kutambua umuhimu wa hifadhi hiyo.

Vilevile Kamishna Meing’ataki aliongeza kuwa kiingilio walichotoa washiriki hao zaidi ya 300 kimeongeza mapato kwa Serikali na kukuza uchumi, fedha ambazo zitatumiwa na Serikali katika kuimarisha sekta mbalimbali nchini.

Kwa upande wake, Mratibu wa Marathon hiyo Mony Luvanda, amesema, Marathon hiyo imelenga kujenga utamaduni wa kufanya mazoezi mara kwa mara, kuitangaza hfadhi ya taifa Kitulo pamoja na kufungua fursa ya kuitangaza wilaya ya Makete, huku ikichochea ongezeko la mapato kwa jamii zinazozunguka hifadhi hiyo na wilaya ya Makete kwa ujumla.

Kitulo Garden Marathon imehusisha mbio za kilomita 5, 10 na 21, zikivutia washiriki wengi na kuleta ushindani wenye tija. Ambapo washindi wa mbio hizo walizawadiwa zawadi mbalimbali, huku washindi watatu wa kwanza kupewa fursa ya kulala na kutalii ndani ya hifadhi ya Taifa ya Kitulo pamoja na wenza wao kwa muda wa siku mbili.