Na Mwandishi wetu, Timesmajira Online, Mbeya
Wizara ya Afya imezindua kamati ya ushauri ya mfumo wa usajili wa saratani katika kanda ya Mbeya kwa ajili ya kumbukumbu ya visa vya ugonjwa huo, hatua inayolenga kuboresha upatikanaji wa takwimu sahihi zitakazosaidia katika maboresho ya huduma na utungaji wa sera za matibabu nchini.
Akizindua kamati hiyo mkoani Mbeya, Kaimu Mkurugenzi wa kitengo cha magonjwa yasiyoambukiza (NCD) kutoka Wizara ya Afya, Edith Bakari, amesema mfumo huo unalenga kutatua changamoto ya muda mrefu ya ukosefu wa taarifa kamili kutoka vituo vya afya vya msingi.

Amesema licha ya mafanikio yanayoonekana katika hospitali za kanda na mikoa, bado kuna pengo la taarifa kutoka ngazi ya msingi, hali inayokwamisha upangaji sahihi wa huduma za afya kwa wagonjwa wa saratani.
“Licha ya mafanikio yaliyopatikana, kamati hii inakwenda kuhakikisha takwimu zinakusanywa kwa ubora na kwa wakati ili kutusaidia katika kupanga sera sahihi za matibabu ya saratani,” amesema Bakari.
Kwa upande wake, Mratibu wa magonjwa yasiyoambukiza mkoani Mbeya, Dkt. Reinfridy Chombo, akimwakilisha Mganga Mkuu wa Mkoa, amesema uzinduzi huo ni hatua muhimu kwa maendeleo ya sekta ya afya mkoani humo.
Amesisitiza kuwa wataalamu waliochaguliwa wanapaswa kufanya kazi kwa bidii na weledi ili kuiwezesha serikali kupanga mipango madhubuti ya kutoa huduma bora zaidi kwa wananchi.

Naye Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Mbeya (MZRH), Dkt. Lazaro Mboma, amesema kamati hiyo imekuja wakati muafaka wakati hospitali hiyo ikiendelea kuboresha huduma za kibobezi za saratani.
Uzinduzi huo ulioshirikisha wadau wa afya, wakiwemo Shirika la Afya Duniani (WHO) na Vital Strategies, umehitimishwa kwa wito kwa wanakamati kufanya kazi kwa uadilifu ili mfumo wa usajili ya Mbeya iwe kiungo madhubuti kati ya vituo vya huduma na mfumo wa taifa wa takwimu.
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani(WHO) kupitia tathmini ya kimataifa ya saratani (GLOBOCAN), saratani inaendelea kuwa miongoni mwa magonjwa yanayoongezeka kwa kasi nchini Tanzania, ambapo zaidi ya wagonjwa 40,000 hugundulika kila mwaka huku idadi ya vifo ikikadiriwa kufikia zaidi ya 27,000. Takwimu hizo zinaonesha pia kuwa saratani zinazoongoza kwa wanawake ni ya mlango wa kizazi na matiti, wakati kwa wanaume ni saratani ya tezi dume, hali inayochangiwa kwa kiasi kikubwa na kuchelewa kugundua ugonjwa pamoja na upatikanaji mdogo wa huduma za uchunguzi wa mapema.
Hata hivyo ripoti ya hivi karibuni ya wizara ya afya Tanzania pamoja na wadau wa afya inaonesha kuwa zaidi ya asilimia 70 ya wagonjwa wa saratani nchini hufika hospitalini wakiwa tayari katika hatua za mwisho za ugonjwa, jambo linalopunguza uwezekano wa matibabu kufanikiwa.

More Stories
DCEA yateketeza ekari 68 za bangi Tabora
Wajumbe wa Bodi ya REA waipongeza ETDCO
Bodi ya REA yaridhishwa na kasi ya usambazaji umeme Mbeya