Na Judith Ferdinand, Mwanza
HALMASHAURI ya Manispaa ya Ilemela mkoani Mwanza imefanikiwa kufikia asilimia 100 ya wanafunzi wa kidato cha kwanza kuripoti katika shule walizopangiwa kwa mwaka wa masomo 2026.
Jumla ya wanafunzi 11,348 walipangiwa kujiunga na kidato cha kwanza, wakiwemo wavulana 5,474 na wasichana 5,874 katika shule za sekondari za halmashauri hiyo, ambao walianza kuripoti Januari na zoezi hilo kukamilika Machi 31, 2026, likitanguliwa na maandalizi ya awali yaliyofanyika ili kuhakikisha kila mwanafunzi anafika shuleni kwa wakati.
Akizungumza na Majira ofisini kwake Aprili 24,2026,Ofisa Elimu Sekondari wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela,Mwalimu Sylvester Mlimi,amesema maandalizi hayo yalianza Desemba kwa kuunda timu za kupokea wanafunzi na kutoa fomu kwa wazazi kabla ya kufunguliwa kwa shule.
Amesema pia halmashauri ilitumia magari ya matangazo mitaani,Wenyeviti wa mitaa na Watendaji wa Kata kuhamasisha wazazi kuhakikisha watoto wao wanaripoti shuleni kwa wakati.
Mlimi ameeleza kuwa wanafunzi waliruhusiwa kuanza masomo hata kama hawajakamilisha sare za shule, huku taratibu za ukamilishaji zikiendelea pia kulikuwa na utaratibu wa kuwasaidia wazazi ambao watoto wao waliopangiwa shule za mbali kubadilisha vituo.Pia kila siku shule zilitoa taarifa za mahudhurio ya wanafunzi, hatua iliyosaidia halmashauri kufanya ufuatiliaji wa karibu na kutoa msukumo pale ilipobidi.
Amesema mafanikio hayo yametokana na ushirikiano wa wazazi na wadau huku halmashauri ikiwa na shule 35 ambapo 34 zinapokea wanafunzi wa kidato cha kwanza,ambapo uwezo wa shule hizo upo vizuri ndio maana wanafunzi wote wamepokelewa kama ilivyopangwa, miundombinuna mazingira ya kusoma ni mazuri,walimu wapo kwa kila shule.
“Kwa kufanya hivyo tumefanikiwa kabla ya Machi 31,2026, watoto wote asilimia 100 wa kidato cha kwanza walikuwa wameisha ripoti shuleni na wapo wanaendelea na masomo yao kama kawaida,”amesema Mwalimu Mlimi.
Hata hivyo amesema, halmshauri hiyo imejipanga kuhakikisha wanafunzi hao wa kidato cha kwanza wanamaliza elimu yao ya sekondari kwa kila shule inakuwa na walimu mahiri kwa ajili ya kuwafundisha.
“Watoto hao ni wadogo,wamezoea kuishi mazingira ya shule ya msingi ambao wanatumia lugha ya Kiswahili.Tunahakikisha tunapanga walimu wenye weledi ambao watawalea,kuwasikiliza na kuwavumilia,lengo ni kuwapa motisha wanafunzi hao waone suala la kujifunza kwao ni la msingi,”.
Sanjari na hayo amesema,wanakuwa na vikao vya wazazi ambavyo wanavisimamia kwa kila shule,ili kuwafahamisha kuwa suala la mtoto kuendelea na masomo ni la kisheria na kiuratibu siyo hiari,hivyo mtoto kwenda shule,maana yake ni fursa na haki yake,hivyo aliwaomba wazazi watoe ushirikiano Kwa kuwahimiza watoto wao kwenda shule Kwa wakati.
“Kwa mzazi ambaye hanaelekea kutuangusha au kutukwamisha, tunachukua hatua kwa kushirikiana na ofisi ya Mkuu wa Wilaya.Serikali imeandaa miundombinu mizuri ya shule na kuajiri walimu hivyo,hatuna sababu ya kukwamisha wanafunzi kwenda shule,”.

More Stories
Airtel yazindua mnara wa 4G Mtwara Vijijini, kuongeza upatikanaji wa intaneti
Airtel Money yaongeza kasi ya ujumuishi wa fedha na uwezeshaji wa kiuchumi kwa Mama Lishe
Wahimizwa kutumia zahanati ya Polisi Mabatini