Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online- Manyoni
IMEELEZWA kuwa hospitali ya Wilaya ya Manyoni mkoani Singida imekuwa na uwezo wa kutoa huduma za afya kutokana na uwepo wa dawa na vifaa tiba vya kisasa ilivyopata kutoka Bohari ya Dawa (MSD).
MSD imeipatia hospiali hiyo vifaa hivyo ambavyo vimeiwezesha kurahisisha huduma kwa wateja(wagonjwa) na kurahisha kazi kwa watoa huduma.

Miongoni vya vifaa tiba hivyo, ni kipimo chenye uwezo wa kupima sampuli nane kwa wakati mmoja, ambacho kimesaidia kupunguza msongamano wa wagonjwa.
Akizungumza na Wahariri wa vyombo vya habari waliotembelea hospitali hiyo mwishoni mwa wiki, Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni Dkt. Bwire Robert, alisema MSD wamefanya mageuzi ya kiutendaji kwa usambazaji wa dawa na vifaa tiba katika hospitali, vituo vya afya na zahanati nchini.
Amesema mabadiliko yaliofanywa na MSD yamewarahisishia wao kama watoa huduma za afya kwa wananchi kufanyakazi zao kwa kujiamini huku malalamiko ya wananchi kuhusu huduma yakipungua kwa kiasi kikubwa.
Kwa mujibu wa Dkt.Bwire kwa sasa MSD wanafanyakazi kidijitali jambo ambalo linarahisisha hadi zahanati kutoa oda ya dawa na kufanyiwa kazi ndani ya muda mfupi na kupatiwa dawa na vifaa tiba.
“Kumekuwa na mapinduzi makubwa katika utoaji huduma kutokana na Serikali kuwekeza katika vifaa tiba, dawa na watoa huduma,”amesema.
Pia amesema uamuzi wa MSD kuwezesha uwepo wa chumba maalum na vifaa tiba kwa ajili ya kuhudumia watoto njiti, umesaidia sasa watoto hao kuhudumiwa vema na kukua bila changamoto yoyote,ambapo kwa sasa hata mtoto mwenye gramu 600 wana uhakika wa kuhudumiwa na kuwa salama.
“MSD imetuletea vifaa maalum vya kuwatunzia watoto njiti,uwepo wa vifaa hivyo umepunguza vifo vya hao kwa asilimia 90.Haya ni mafanikio makubwa katika sekta ya afya,tunaipongeza Serikali yetu inayoongozwa na Rais Samia kwani kupitia MSD huduma za afya zimekuwa bora na za uhakika,”amesema.
Sanjari na hayo amesema,MSD imewezesha hospitali ya Wilaya ya Manyoni kuwa na vifaa vya maabara vya kisasa ikiwemo
mashine za UtraSound ya kisasa, mashine za upasuaji,mashine ya usingizi,pia wanavyo vya kutosha vitanda vyenye mashine za kupumulia,huku alisisitiza kuwa uamuzi wa MSD kujenga chumba cha kisasa cha kuhifadhia maiti imesaidia miili ya wapendwa kuhifadhiwa sehemu salama katika hospitali hiyo.

Meneja MSD Kanda ya Dodoma,Mwanashehe Jumaa, amesema MSD inahudumia vituo zaidi ya 400 kwa Mkoa wa Singida huku Kanda Nzima ya Kati ikiwemo Mkoa wa Singida, Dodoma na Wilaya ya Kiteto ikiwa na jumla ya vituo zaidi ya 840.
Kwa wa upande wa wananchi wa Wilaya ya Manyoni,wameipongeza Serikali kupitia MSD kwa kuendelea kuboresha huduma za afya kwa kuiwezesha hospitali ya wilaya hiyo kuwa na vifaa tiba vya kisasa na uhakika wa dawa kwani yale malalamiko ya kukosa huduma hayapo tena na kwa sasa kimbilio lao ni katika hospitali za Serikali.


More Stories
Airtel yazindua mnara wa 4G Mtwara Vijijini, kuongeza upatikanaji wa intaneti
Airtel Money yaongeza kasi ya ujumuishi wa fedha na uwezeshaji wa kiuchumi kwa Mama Lishe
Wahimizwa kutumia zahanati ya Polisi Mabatini