Na Martha Fatael, TimesMajira Online
Mama mjasiriamali Anna Mwenda, mfanyabiashara wa mboga mboga katika soko la Manyema, Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro, amesema biashara hiyo imekuwa tegemeo kuu la kuiendesha familia yake huku akikabiliwa na changamoto mbalimbali za kiuchumi na kijamii.
Amesema hulazimika kuanza shughuli zake usiku wa manane ili kuwahi sokoni kupata mboga moja kwa moja kutoka kwa wakulima, hatua inayomsaidia kuepuka bei kubwa kutoka kwa madalali, ingawa bado hukutana na changamoto za usalama na uchovu kutokana na ratiba ngumu ya kazi.

Anna amesema licha ya kupata faida inayobadilika kulingana na hali ya soko, amekuwa akibeba majukumu makubwa ya kifedha katika familia ikiwemo kulipia mahitaji yote muhimu, hali inayoongeza presha kutokana na kukosa msaada wa kutosha nyumbani.
Hata hivyo, amesema hupata nguvu kupitia ushirikiano wa wanawake wenzake sokoni, ambao hutiana moyo na kusaidiana katika kukabiliana na changamoto za maisha ya kila siku.
Kwa upande wake, Meneja wa Mafunzo na Usimamizi wa CRB, Joshua Mwakalobo, amesema Benki ya CRDB imeanzisha programu ya “mikopo nafuu kwa wajasiriamali wa mboga mboga” inayolenga kuwapatia mikopo isiyo na riba pamoja na elimu ya kifedha ili kuwawezesha kukuza mitaji yao.

Amesema programu hiyo inayofadhiliwa na benki hiyo kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo inalenga kuwafikia wajasiriamali wadogo wengi zaidi, hasa wanawake walioko katika sekta isiyo rasmi, ili kuboresha biashara zao na kuinua vipato vyao.
Awali, Mkurugenzi wa Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA), Rose Reuben, amesema taasisi hiyo imeendelea kuwajengea uwezo wanawake kiuchumi kupitia mafunzo ya ujasiriamali na usimamizi wa kipato ili waweze kufanya maamuzi sahihi katika shughuli zao.
Amesema pia bado kuna changamoto ya ukatili wa kijinsia wa kiuchumi unaowakumba wanawake wengi, hali inayowarudisha nyuma katika maendeleo yao, hivyo kusisitiza umuhimu wa elimu na uelewa ili kuwawezesha kujikwamua na kujenga maisha bora zaidi.

More Stories
NMB ilivyosaidia Serikali kukusanya zaidi ya Sh trilioni 9.8
Serikali yaongeza nguvu kwa wachimbaji wadogo,yasisitiza usalama Migodini
REA imeleta mageuzi sekta ya nishati