Judith Ferdinand, Timesmajira Online-Mwanza
UONGOZI wa Mtaa wa Nyamanoro Mashariki,wilayani Ilemela mkoani Mwanza, umejipanga kushirikiana na wananchi kuboresha barabara kuu ya mtaa huo ya Sinza- Mjimwema,yenye urefu wa takribani nusu kilomita ambayo inategemewa na kaya takribani 1,200.
Ambapo ujenzi huo ni muendelezo kwani mwaka jana mwanzoni uongozi huo kwa kushirikiana na wananchi pamoja na wadaua,walianza kuijenga kipande cha barabara hiyo kwa kiwango cha zege ili iweze kupitika wakati wote wa mwaka.
Akizungumza na Majira Machi 31,2026 ,Mwenyekiti wa mtaa huo, Missa Budundu, amesema waliku wanasubiri mvua zipungue hivyo mara baada ya sikukuu ya Pasaka, wananchi kwa kushirikiana na viongozi wataanza kwanza kukarabati maeneo yaliyoharibika, ambapo shughuli hizo zitafanyika kila Jumamosi.
Budundu amesema,mtaa huo utaanza tena ukusanyaji wa michango ya fedha kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa barabara hiyo, baada ya shughuli hizo kusitishwa kwa muda kutokana na uhaba wa fedha za ununuzi wa malighafi hususani saruji na vitendea kazi vingine.Barabara hiyo ni ya wananchi, na ujenzi wake unategemea ushirikiano wa wadau pamoja na michango ya wakazi wenyewe.
“Kupitia mikutano ya hadhara, tulikubaliana kila kaya ichangie shilingi 2,000.Hadi sasa, taarifa ya mradi huu imewasilishwa pia katika Kamati ya Maendeleo ya Kata,pia kwenye Halmashauri ili kupata uwezekano wa msaada zaidi katika juhudi hizo za maendeleo,”amesema Budundu.
Kwa upande wake, mkazi wa mtaa huo, Yohana Aloyce,amesema barabara hiyo ni muhimu kwa wananchi, hasa wafanyabiashara wanaotegemea usafirishaji wa bidhaa kufika katika maduka yao kwa urahisi.Kwani mvua zilizonyesha hivi karibuni zimeharibu sehemu kubwa ya barabara hiyo, hali iliyosababisha kuwepo kwa mawe mengi na kufanya usafirishaji wa bidhaa kuwa mgumu zaidi.
Naye mwendesha bodaboda kutoka mtaa huo, Alex Antila,amesema ubovu wa barabara hiyo unaathiri pia vyombo vya moto, hususani pikipiki, kwa kusababisha uharibifu wa mara kwa mara wa vifaa kama ‘shocker’,pia inaweza kusababisha na ajali.
Kwa upande wake, Elizabeth Kalonga amesema hali ya barabara hiyo imekuwa kero kwa watembea kwa miguu, hasa wazee na watoto, kutokana na jiografia ya eneo hilo kuwa ya mlimani na yenye mawe mengi.
“Kabla ya mvua kunyesha, barabara ilikuwa inapitika vizuri na tuliweza kutumia usafiri mbalimbali kama magari na pikipiki kufika nyumbani. Hali hiyo ilirahisisha hata huduma za dharura kama kuwafikisha katika vituo vya kutolea huduma wagonjwa na wajawazito,”amesema Kalonga.

More Stories
NMB ilivyosaidia Serikali kukusanya zaidi ya Sh trilioni 9.8
Serikali yaongeza nguvu kwa wachimbaji wadogo,yasisitiza usalama Migodini
REA imeleta mageuzi sekta ya nishati