







Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma
WAZIRI Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba,amewaongoza waombolezaji kuaga mwili wa aliyekuwa Waziri wa Nchi,ofisi ya Waziri Mkuu ,Sera,Bunhe Uratibu na wenye Ulemavu William katika viwanja vya Bunge jijini Dodoma.
Amesema kuondoka kwa aliyekuwa kiongozi na mtumishi wa umma Lukuvi, ni pigo kubwa kwa Taifa na kumeacha simanzi miongoni mwa Watanzania kutokana na utendaji wake.
Akizungumza leo Machi 27, 2026 katika viwanja vya Bunge jijini Dodoma wakati wa misa ya kuaga mwili wa Lukuvi huyo Dkt. Nchemba amesema Watanzania ,familia wameachwa na butwaa kubwa kutokana na mchango mkubwa alioutoa Lukuvi kwa Taifa.
Amesema kuwa marehemu alikuwa mtu wa mawasiliano ya karibu na viongozi wenzake hadi siku za mwisho za maisha yake, akifuatilia kwa karibu ratiba na majukumu ya kazi licha ya changamoto za kiafya.
“Kuondoka kwake ni simanzi kubwa,tumempoteza kiongozi aliyekuwa na uzalendo wa hali ya juu, busara, ukomavu wa kisiasa na uwezo mkubwa wa uratibu wa shughuli za Serikali,” amesema.
Dkt. Nchemba ametoa pole kwa familia, ndugu, jamaa na marafiki wote walioguswa na msiba huo, akisisitiza kuwa Lukuvi atakumbukwa kwa mengi mema aliyoyafanya katika utumishi wake uliotukuka.
Ameongeza kuwa Serikali imepoteza mshauri muhimu ambaye alikuwa msaada mkubwa kwa mawaziri na viongozi mbalimbali, akiwalea na kuwasaidia kuboresha utendaji wao katika sekta walizokuwa wakizisimamia.
“Alikuwa mlezi wa kila mmoja,alipenda kusaidia mawaziri ili kuhakikisha wanafanikiwa katika majukumu yao, nidhamu yake ya kazi na uwezo wa kutekeleza majukumu ndiyo iliyowafanya Marais mbalimbali kuona anafaa kuendelea kulitumikia Taifa,” amesema.
Waziri Mkuu huyo alibainisha kuwa yeye binafsi ni miongoni mwa watu walionufaika na busara za marehemu, akieleza kuwa alimshauri tangu alipokuwa Mbunge hadi alipoteuliwa kuwa Waziri wa Fedha.
“Mnyonge mnyongeni lakini katika masuala ya uratibu, Lukuvi alikuwa kama “profesa,” akihakikisha mahusiano kati ya Serikali na Bunge yanakuwa imara, pamoja na kudumisha uhusiano mzuri kati ya wabunge, wananchi na Serikali.”amesisitiza
Aidha, alimshukuru Paroko wa Parokia ya Bikira Maria Kisasa Sostenes Ndendya aliyeongoza ibada hiyo ya kuaga mwili kwa ujumbe wa mahubiri uliotoa faraja na elimu kwa waombolezaji, akisema amejawa na huzuni kubwa kufuatia kumpoteza kiongozi huyo katika kipindi ambacho walikuwa wamepanga kutekeleza mambo mengi ya maendeleo ya Taifa.
“Serikali itaendelea kuwa bega kwa bega na familia ya marehemu kama ilivyofanya tangu alipopata changamoto ya kiafya,” alisisitiza.
Naye Makamu wa Rais Mstaafu, Dk. Philip Mpango amdsema katika kipindi hiki mitandao haitumiwi vizuri hivyo akiwasii familia ya marehemu Lukuvi isife moyo licha ya maneno mengi yanayosemwa mitandaoni juu ya mpendwa awao.
Amesema alikuwa ni hazina wamemtumia mara nyingi kufunda mawaziri kuwakumbusha wajibu wao ndani ya bunge na ndani ya serikali.
Akiwa mchanga katika siasa na Waziri wa fedha na kipindi vyuma vilipobana alimuelekeza nyakati zote namna ya Kuendesha shughuli zake ndani ya bunge na serikali.
“Alikuwa mtu mwema, aliyependa kushuri wenzake juu ya utendaji kazi wao, huku akimwmabia kuwa tangu uhuru hajawahi kutokea waziri wa fedha bahili kama wewe, hiyo ilinifanya kuona kazi yangu ni rahisi,”amesisitiza Dk.Mpango
Akizungumzia marehemu Lukuvi, Mwanasheria Mkuu wa Serikali George Masaju amesema alikuwa na uwezo mkubwa wa kujenga mahusiano, nafasi ya mnadhamu wa Bunge ambaye ni msimamizi wa shughuli za bunge ambayo marehemu ameishika kwa vipindi virefu kuliko mawaziri wote ilitaka mtu mwenye sifa kama zake.
Amesema marehemu Lukuvi alikuwa mwepesi wa kujifunza, anayeshaurika , mchapakazi, muadikifu na muaminifu.
Misa hiyo imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali, wabunge, ndugu na wananchi waliojitokeza kutoa heshima zao za mwisho kwa marehemu Lukuvi.
Lukuvi ambaye alikuwa Waziri wa Nchi,Ofisi ya Waziri Mkuu,Sera,Bunge,Uratibu na Wenye Ulemavu amefariki Machi 25,2026 katika hospitali ya Benjamini Mkapa alikokuwa akipatiwa matibabu baada ya kupata tatizo la mshtuko wa moyo.

More Stories
NMB ilivyosaidia Serikali kukusanya zaidi ya Sh trilioni 9.8
Serikali yaongeza nguvu kwa wachimbaji wadogo,yasisitiza usalama Migodini
REA imeleta mageuzi sekta ya nishati