Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online-Sikonge
MABINTI zaidi ya 34 waliokosa fursa ya kupata elimu ya sekondari wilayani Sikonge mkoani Tabora wameishukuru Serikali kwa kuwapa fursa ya kupata elimu hiyo kwa miaka miwili pasipo kulipa gharama yoyote.
Mabinti hao ambao wengi wao walikatishwa masomo kwa sababu mbalimbali ikiwemo hali duni ya maisha ya wazazi wao, kupata ujauzito, kukatishwa masomo ili waozeshwe katika umri mdogo na mtizamo hasi ya wazazi wao kuhusu elimu.
Watoto hao licha ya kupata fursa ya kusoma elimu ya sekondari bure kwa miaka 2 (QT) pia wanasoma masomo ya ufundi stadi ambapo kila mmoja anasoma fani anayopenda, hii inampa fursa ya kupata elimu ya sekondari na ujuzi wa ufundi pia.
Hayo waliyabainisha wakati wakizungumza na waandishi wa habari waliotembelea Chuo cha Maendeleo ya Wananchi (FDC),wilayani humo.
Miracle Mvungu (25) kutoka Kata ya Igigwa wilayani humo ameeleza kuwa baada ya kumaliza darasa la saba alishindwa kuendelea na masomo ya sekondari kutokana na uwezo mdogo wa wazazi wake hivyo ndoto yake ya kuwa nesi ikakatishwa.
‘Tunamshukuru sana mama yetu, Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kutuonea huruma na kuanzisha program hii ya elimu kwa walioikosa, ndoto yangu ya kuwa nesi ilikuwa imekufa, sasa nitasoma kwa bidii ili nifikie ndoto yangu’, amesema.
Clemencia Athuman (20) kutoka Kijiji cha Ipole wilayani humo aliyekatisha masomo akiwa kidato cha kwanza baada ya kushawishiwa na mama yake, amesema fursa hiyo ni muhimu kwake hivyo atasoma kwa bidii ili awe mwalimu.
Mkuu wa chuo hicho,Gaston Chiwalanga, amesema Serikali imetoa fursa kwa watoto wa kike wote waliokosa elimu ya sekondari katika wilaya hiyo na wilaya nyingine zote nchini kujiandikisha ili waingizwe katika programu hiyo.
Amesisitiza kuwa program hiyo ni endelevu katika kipindi hiki cha utawala wa Rais Samia na Serikali inagharamia kila kitu, hivyo akatoa wito kwa wazazi, walezi na jamii kwa ujumla kuleta mabinti waliokosa fursa hiyo kujiunga na chuo hicho.
Aidha amedokeza kuwa Rais Samia ametoa fursa kwa vijana wa kiume na kike nchi nzima kujiunga Vyuo vya Ufundi Stadi-VETA na FDC kupitia Programu ya Ofisi ya Waziri Mkuu ili kupata ujuzi utakaowawezesha kujiajiri au kuajiriwa.
Chiwalanga ameeleza kuwa Serikali inagharamia kila kitu katika mafunzo hayo, kila kijana anachagua fani anayotaka kusoma, baadhi ya fani hizo ni ufundi umeme, magari, mabomba, ushonaji, uungaji vyuma na uashi.

More Stories
NMB ilivyosaidia Serikali kukusanya zaidi ya Sh trilioni 9.8
Serikali yaongeza nguvu kwa wachimbaji wadogo,yasisitiza usalama Migodini
REA imeleta mageuzi sekta ya nishati