April 23, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali:Hatutasita kuchukua hatua kwa wafanyabiashara wanaoficha mafuta

Na Penina Malundo,Timesmajira

SERIKALI imesema haitasita kuchukua hatua kali dhidi ya mfanyabiashara yeyote atakayebainika kuficha mafuta kwa lengo la kuyauza baadaye kwa bei ya juu.

Aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam,Katibu Mkuu Wizara ya Nishati anayeshughulikia Mafuta na Gesi Asilia, Dkt. James Mataragio, wakati wa ziara ya kutembelea maghala ya kuhifadhia mafuta ya Kampuni ya Camel Oil yaliyopo Kurasini, jijini Dar es Salaam, ikiwa ni sehemu ya jitihada za Serikali kufuatilia hali ya upatikanaji wa mafuta nchini.

Dkt.Mataragio amesema vitendo hivyo vya ufichwaji wa mafuta havitavumiliwa na Serikali kwani tayari wamesikia kelele kwa baadhi ya vituo kuwa havipati mafuta na vingine kunaucheleweshaji wa makusudi katika upakiaji.

“Ziara hii imekuja makusudi kwenye kampuni hii ya Cameil Oil kujionea hali halisi. Serikali inataka kuhakikisha mafuta yanapatikana na yanafika katika vituo vyote nchini,” alisema Dkt.Mataragio

Amesema miongoni mwa lengo la kufanya ziara hiyo ni kujiridhisha kuhusu uwepo wa akiba ya mafuta na mwenendo wa usambazaji wake, kufuatia malalamiko kutoka kwa baadhi ya vituo vya mafuta vinavyodai kucheleweshewa huduma au kutopata mafuta kwa wakati.

Amesema Serikali imelenga kuhakikisha nchi inakuwa na akiba ya kutosha ya mafuta, huku akibainisha kuwa hakuna uhaba wa mafuta kwa sasa na yanatosheleza mahitaji ya wananchi.

Katika hatua nyingine, Dkr.Mataragio amewapongeza Kampuni ya Camel Oil kwa kuendelea kutoa huduma usiku na mchana, akiwataka kudumisha hali hiyo hasa katika kipindi hiki ambacho baadhi ya wafanyabiashara wanajaribu kutumia fursa ya soko kujinufaisha kwa njia zisizo halali.

Amesema vita inayoendelea Mashariki ya Kati, imeathiri soko la mafuta duniani, lakini kwa Tanzania imejipanga vyema na ina akiba ya kutosha inayoweza kuhudumia nchi hadi mwezi Julai mwaka huu.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa EWURA, Dk. James Andilile, amesema changamoto za upatikanaji wa mafuta duniani zimetokana na athari za vita hiyo, akibainisha kuwa Tanzania inaagiza sehemu kubwa ya mafuta kutoka Mashariki ya Kati.

Amesema serikali ilichukua hatua mapema kuhakikisha upatikanaji wa mafuta unaendelea kuwa salama, huku akisisitiza kuwa hakuna uhaba wa mafuta nchini kwa sasa.

Hata hivyo, amesema za kuwa kuongezeka kwa gharama za usafirishaji na uagizaji mafuta kutokana na uharibifu wa miundombinu katika maeneo ya vita kumeongeza gharama za mafuta katika soko la dunia, hali inayoweza kuathiri upangaji wa bei nchini.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Camel Oil, Salrh Bajber, amesema kampuni hiyo inaendelea kutoa huduma kama kawaida na ina akiba ya kutosha ya mafuta.

Amesema kuwa kwa mwezi Aprili wameagiza lita milioni 70 za mafuta kwa ajili ya maghala yao, huku kwa mwezi Mei wakitarajia kuingiza lita milioni 84 kwa ajili ya usambazaji.

Aidha, amesema hadi Machi 25, 2026, kampuni hiyo imesambaza zaidi ya lita milioni 44 za mafuta, huku ikiwa na oda zinazoendelea za takribani lita milioni tano ambazo ziko katika hatua za upakiaji.