April 23, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Zaidi 200,000 kupatiwa chanjo ya Polio Mwanza

Judith Ferdinand, Timesmajira Online-Mwanza

HALMASHAURI ya Jiji la Mwanza, katika siku nne za kampeni maalumu ya chanjo ya polio kwa mikoa saba ilioanza Machi 24 hadi 27,2026, inatarajia kuwafikia watoto zaidi ya 200,000 wenye umri chini ya miaka 10,kwa awamu ya kwanza ili kuwakinga na ugonjwa wa polio ambao vimelea vyake vimetajwa kubainika katika Mkoa wa Mwanza.

Akizungumza Machi 24,2026 na wananchi katika kituo cha afya cha Mkolani jijini Mwanza,Ofisa Tawala wa Halmashauri y hiyo, Magreth John,licha ya kuhamasisha wazazi kutoa ushirikiano kwa wataalam watakaopita katika maeneo yao kutoa chanjo hiyo pia alieleza umhimu wa chanjo hiyo kwa watoto.

“Chanjo hii tutaifanya hata kwa wale watoto waliokuwa wamepata chanjo ya mwanzo ya polio,tunaifanya kwa sababu kuna viashria ambavyo vimeweza kuonekana,”amesema Magreth na kuongeza:

“Zoezi hili ni la kwetu hivyo viongozi wa Serikali za mtaa ni wajibu wao kuhamasisha wananchi waweze kupokea chanjo hiyo, lakini watoto wetu tuhakikishe kuanzia miaka 0 hadi 10 wanapata chanjo hii,”.

Akizungumza kwa niaba ya Mganga Mkuu wa Mwanza, Mfamasia wa Jiji la Mwanza, Gipson Simburya,amesema tafiti zilizofanyika hivi karibuni ziliibaini uwepo wa vimelea vya ugonjwa huo ambapo mtoto asipopatiwa chanjo husabisha kupooza viungo vya mwili na kusababisha ulemavu wa kudumu na wakati mwingine kupoteza maisha.

” Madhara anayoweza kupata mtoto mwenye vimelea vya polio ni kupooza, miguu inakuwa legelege na wakati mwingine kusababisha kifo”amesema Simburya.

“Chanjo itatolewa kwa muda wa siku nne , tutapita katika maeneo ya shuleni na nyumba kwa nyumba kuhakikisha watoto wote wanapatiwa chanjo, tuwaombe wazazi watoe ushirikiano ili kumkinga mtoto dhidi ya vimelea hivyo,”.

Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Mkolani,John Mbira,ameaema wamejitahidi kuhamasisha wananchi kushiriki zoezi hilo na kuwa mabalozi kwa wengine wenye imani potofu kuhusiana na chanjo hiyo.