Judith Ferdinand, Timesmajira Online-Mwanza
SHIRIKA la Ladies Joint Forum (LJF), kwa kushirikiana na Kijiweni Production, limeutambulisha rasmi mradi wa Paza Mwendo wilayani Misungwi, mkoani Mwanza, ukiwa na lengo la kuwawezesha wanawake katika sekta ya utengenezaji wa filamu za makala bunifu.
Akielezea malengo ya mradi huo, Mkurugenzi wa LJF, Fransisca Mboya,amesema mpango huo unalenga kuwajengea uwezo wanawake watengeneza filamu pamoja na madereva bajaji wanawake, ili waweze kusimulia hadithi zao kupitia kazi za ubunifu.

Amesema awamu ya kwanza itawahusisha wanawake sita kutoka mikoa ya Dar-es- Salaam na Mwanza, ambao watapatiwa mafunzo maalum ya kuandaa makala zenye ubunifu, wakianza kwa kuangazia maisha ya wanawake madereva bajaji waliopatikana kupitia mradi wa She Drives to Change.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kijiweni Production, Amil Shivji,amesema walivutiwa kushiriki katika mradi huo baada ya kufahamu juhudi za kuwawezesha wanawake madereva bajaji, na hivyo kuona umuhimu wa kuyaweka wazi maisha yao kupitia makala zitakazotengenezwa na wanawake wenyewe.
Awali, akifungua warsha ya mafunzo hayo, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi, Dkt. Shami Chrispin,amepongeza wadau hao kwa kuleta mradi huo na kuahidi ushirikiano kutoka kwa halmashauri, ikiwemo uwezekano wa wanufaika kupata mikopo kupitia asilimia 10 ya mapato ya ndani inayotengwa kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.
Mradi wa Paza Mwendo unatekelezwa chini ya mpango wa Vijana@Work, ukisimamiwa na Goethe-Institut Tanzania kwa kushirikiana na Culture and Development East Africa, kwa ufadhili wa Umoja wa Ulaya.
Kupitia mradi huu, wanawake watengeneza filamu na madereva bajaji wanakutana ili kuunda makala bunifu zinazosimulia maisha yao ya kila siku, hatua inayotarajiwa kuongeza sauti na ushiriki wa wanawake katika sekta ya ubunifu na maendeleo ya kijamii.


More Stories
NMB ilivyosaidia Serikali kukusanya zaidi ya Sh trilioni 9.8
Serikali yaongeza nguvu kwa wachimbaji wadogo,yasisitiza usalama Migodini
REA imeleta mageuzi sekta ya nishati