NA Joyce Kasiki, Dodoma
MTAKWIMU Mkuu wa Serikali, Dkt. Amina Msengwa, ametangaza kuanza kwa tafiti nne muhimu za kitaifa zitakazokusanya takwimu za kina kuhusu shughuli za biashara, sekta isiyo rasmi, huduma za fedha kwa wafanyabiashara wadogo na uzalishaji viwandani, hatua inayolenga kuimarisha mipango ya maendeleo ya kiuchumi nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma, Dkt. Msengwa amesema kuwa kwa mujibu wa Sheria ya Takwimu Sura ya 351, Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) imepewa jukumu la kuratibu na kusimamia uzalishaji wa takwimu rasmi nchini.
Amesema kazi za uwandani zitakazohusisha ukusanyaji wa taarifa za tafiti nne zinazotekelezwa kwa sasa ambazo ni Utafiti wa Kina wa Shughuli za Kibiashara, Utafiti wa Sekta Isiyo Rasmi, Utafiti wa Huduma za Fedha kwa Wafanyabiashara Wadogo Sana, Wadogo na wa Kati (FINSCOPE MSMEs) pamoja na Utafiti wa Uzalishaji Viwandani.
Dkt. Msengwa amesema madhumuni ya tafiti hizo ni kukusanya taarifa muhimu kuhusu shughuli za biashara katika sekta rasmi na zisizo rasmi, ikiwemo uzalishaji viwandani, ajira, uwekezaji na mazingira ya biashara nchini.
Ameeleza kuwa taarifa zitakazopatikana zitaisaidia Serikali pamoja na wadau wa sekta binafsi, mashirika yasiyo ya kiserikali na watafiti kubuni programu mbalimbali za kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini.
Aidha, amesema tafiti hizo zitasaidia kuhuisha takwimu za thamani ya pato ghafi ambalo linaendana na uzalishaji wa bidhaa na huduma mbalimbali, kwa lengo la kubaini mchango wa shughuli hizo za kiuchumi katika Pato la Taifa.
Akifafanua kuhusu Utafiti wa Huduma za Fedha kwa Wafanyabiashara , Dkt. Msengwa alisema utafiti huo utaipatia Serikali takwimu muhimu zitakazotumika kupima maendeleo ya utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Ujumuishaji wa Kifedha Awamu ya Tatu (NFIF III) pamoja na Mpango Mkuu wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha (FSDMP).
Alisema matokeo ya utafiti huo pia yatatoa ushahidi wa kitakwimu kuhusu upatikanaji wa mikopo, akiba, bima na huduma za fedha za kidijitali kwa wafanyabiashara wadogo sana, wadogo na wa kati.
Kwa upande wa Utafiti wa Uzalishaji Viwandani, alisema utafiti huo utawezesha kupatikana kwa viashiria na taarifa mbalimbali ikiwemo orodha ya viwanda vilivyopo katika mikoa mbalimbali, mwaka wa kuanza kwa uzalishaji, aina za bidhaa zinazozalishwa, idadi ya wafanyakazi pamoja na gharama za uzalishaji na mapato yatokanayo na shughuli za uzalishaji.
Ameongeza kuwa taarifa nyingine zitakazokusanywa ni pamoja na masoko, usimamizi wa mazingira, teknolojia ya mitambo, mipango ya uwekezaji na changamoto zinazovikabili viwanda.
Kwa mujibu wa Dkt. Msengwa, taarifa hizo zitawezesha Serikali kuimarisha programu za maendeleo ya ujuzi, pamoja na kupanga sera na mikakati itakayosaidia kuongeza mchango wa sekta ya viwanda katika Pato la Taifa.
Amesema malengo mengine ya tafiti hizo ni kubaini ongezeko la thamani ya bidhaa na huduma zinazozalishwa, kupima tija ya uzalishaji, thamani ya ukuzaji wa rasilimali pamoja na mahusiano ya sekta mbalimbali za kiuchumi.
Dkt. Msengwa ameongeza kuwa matokeo ya tafiti hizo yatasaidia katika utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050, Malengo ya Maendeleo Endelevu ya mwaka 2030 (SDGs), Agenda ya Maendeleo ya Afrika ya mwaka 2063 na Dira ya Afrika Mashariki ya mwaka 2050, hususan katika maeneo yanayohusiana na biashara, sekta isiyo rasmi na maendeleo ya viwanda.
Amesema tafiti hizo zitafanyika nchi nzima katika maeneo 1,518 ya utafiti, ambapo maeneo 703 yatatumika kwa ajili ya Utafiti wa Sekta Isiyo Rasmi na maeneo 815 kwa ajili ya Utafiti wa Finscope.
Aidha, amesema Utafiti wa Kina wa Shughuli za Biashara utahusisha taasisi na biashara 8,624 huku Utafiti wa Uzalishaji Viwandani ukihusisha viwanda 4,245.
Kwa mujibu wake, jumla ya wadadisi 713 na wasimamizi 69 watashiriki katika zoezi la ukusanyaji wa taarifa ili kuhakikisha takwimu zinazopatikana zina ubora wa hali ya juu.
Amesema zoezi la ukusanyaji wa taarifa litachukua takribani miezi miwili kuanzia Machi 11 hadi Mei 10, 2026, na tafiti zote zitatumia teknolojia ya vishikwambi au simu.
Dkt. Msengwa amesisitiza kuwa tafiti hizo zinafanyika kwa mujibu wa Sheria ya Takwimu Sura ya 351 na kwamba taarifa zote zitakazokusanywa zitakuwa siri na zitatumika kwa madhumuni ya kitakwimu pekee.
Pia ameeleza kuwa NBS inaendelea kutekeleza tafiti nyingine muhimu ikiwemo Utafiti wa Watu Wenye Uwezo wa Kufanya Kazi wa mwaka 2026 unaolenga kupata viashiria vya soko la ajira nchini, ikiwemo kiwango cha ukosefu wa ajira na ukubwa wa nguvu kazi.
Amesema utafiti mwingine ni wa kutathmini upatikanaji wa huduma za maji na usafi wa mazingira katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini, ambapo matokeo yake yatasaidia kuandaa mikakati ya kuboresha huduma hizo pamoja na mazingira ya vituo vya afya.
Aidha, amesema kuna Utafiti wa Mifugo unaotekelezwa kwa ushirikiano kati ya NBS, Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) na Benki ya Dunia, unaolenga kupima mbinu mpya za kuhesabu mifugo nchini.
Dkt.Msengwa amesema utafiti huo unatekelezwa katika nchi 30 barani Afrika huku Tanzania ikiwa moja ya nchi za majaribio ambapo mikoa ya Arusha na Tabora itahusika.
“Kutokana na umuhimu wa tafiti hizo, Dkt. Msengwa aliwataka Watanzania watakaofikiwa na wadadisi kutoa ushirikiano kwa kutoa taarifa sahihi ili kusaidia Serikali kupanga mipango ya maendeleo kwa kutumia ushahidi wa kitakwimu.”amesema
Amesema taarifa za kina za tafiti hizo zitatolewa kupitia ripoti zitakazoandaliwa na kuzinduliwa ifikapo mwezi Juni mwaka huu.
Katika hatua nyingine, Dkt. Msengwa amevishukuru vyombo vya habari kwa mchango wao mkubwa katika kuelimisha na kuhamasisha wananchi kushiriki katika tafiti mbalimbali zinazofanywa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu.
Amesema ushirikiano wa karibu na vyombo vya habari umechangia kuongeza mwitikio wa wananchi katika tafiti nyingi zinazofanywa nchini.
Aidha, amewashukuru wadau wote wa tafiti hizo wakiwemo Mfuko wa Kuendeleza Sekta ya Fedha (FSDT), FinMark Trust, Benki ya Dunia na Shirika la Kazi Duniani (ILO) kwa ushirikiano wao katika kufanikisha utekelezaji wa tafiti hizo.

More Stories
Rais Samia na Afisa Mtendaji Mkuu ABF Sugar kuendeleza uwekezaji sekta ya sukari
Msichana Initiative yazindua mradi wa Renewed Women Voices and Leadership Tanzania
Mikopo asilimia 10 yaendelea kuwakomboa wananchi Mbarali